55. Tunawafuata Sunnah na Mkusanyiko na tunajiepusha na mambo ya kinyume

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

87 – Tunafuata Sunnah na mkusanyiko na tunajiepusha na mambo yanayoenda kinyume, kutofautiana na mipasuko.

MAELEZO

Sunnah ni ile njia yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Mkusanyiko ni mkusanyiko wa waislamu ambao ni Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema mpaka siku ya Qiyaamah. Kuwafuata ni uongofu na kwenda kinyume nao ni upotevu.

Tunajiepusha kupondoka kutokana na Sunnah na kutofautiana na Mkusanyiko, ambao wao ndio Salaf. Tofauti na wanavofikiria wengi, sio katika kupondoka muislamu akachagua maoni fulani miongoni mwa maoni ya tofauti kutokana na vile dalili ilivyomdhihirikia, ingawa kikosi kikubwa cha wanazuoni wanaona kinyume na hivo. Kwa sababu hakuna dalili yoyote, si ndani ya Qur-aan wala Sunnah, inayosema kuwa yale wanayoona jopo kubwa la wanazuoni ndio ya sawa kuliko yale wanayoona wale wenye kupingana nao wakati kunapokosekana dalili. Hata hivyo ni lazima kufuata maoni ambayo waislamu wote wameafikiana. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

”Yule atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na ni uovu ulioje mahali pa kuishia!”[1]

Lakini wakati kunapokuwa tofauti basi kilicho cha lazima ni kurejea katika Qur-aan na Sunnah. Yule ambaye itambainikia haki, basi aifuate. Vinginevyo auombe moyo wake fatwa, ni mamoja ameenda sambamba na kikosi kikubwa cha wanazuoni au ameenda kinyume nao. Sifikirii kuwa kuna yeyote anayewafata wanazuoni wengi katika kila kitu ambacho haki haiko wazi. Isipokuwa mara anakuwa hivi na mara nyingine anakuwa hivi, kutegemea vile moyo wake unahisi utulivu na kukunjuka. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi sallam) amesema kweli pale aliposema:

”Uulize fatwa moyo wako hata kama atakupa fatwa mtu.”[2]

[1] 4:115

[2] Nzuri kwa mujibu wa ash-Shawkaaniy katika ”Irshaad-ul-Fuhuul” (2/284).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 80-81
  • Imechapishwa: 08/10/2024