55. Nyepesi zaidi kwenye ulimi na daraja kubwa zaidi

30 – Kushughulika na Dhikr humfanya mja akapewa zawadi bora kuliko anayemuomba. ´Umar bin al-Khattwaab amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amesema: ”Anayeshughulishwa na Dhikr Yangu kiasi cha kushindwa kuniomba, basi Nitampa bora zaidi ya ninayowapa wanaoniomba.”[1]

31 – Ni ´ibaadah nyepesi zaidi kwa viungo lakini yenye daraja kubwa sana. Kwani harakati za ulimi ni nyepesi zaidi kuliko viungo vingine. Lau kiungo kingine kingesogea kama ulimi, basi mja angeliona uzito mkubwa mno.

32 – Ni mimea ya Pepo. ´Abdullaah bin Mas´uud amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nilipokutana na Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika usiku niliyopandishwa mbinguni. Akanambia: ”Ee Muhammad! Wape ummah wako salamu, na waambie kuwa Pepo ni nzuri udongo wake, tamu maji yake, ni tambarare tupu na mimea yake ni:

سبحان الله والحمد لله ولا إله إلا الله والله أكبر

”Allaah ametakasika kutokana na mapungufu, himdi zote njema anastahiki Allaah na Allaah ni mkubwa.”[2]

Jaabir ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule anayesema:

سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيم وبِحَمْدِهِ

”Allaah ametakasika kutokana na mapungufu, Mtukufu na himdi zote njema ni Zake.”

utapandwa kwa ajili yake mtende Peponi.”[3]

33 – Kwamba zawadi na fadhilah zilizopangwa juu yake hazijapangwa juu ya matendo mengine. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kusema:

لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌم

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana na mshirika. Ufalme Wake na himdi Zake na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.”

mara mia kwa siku, basi analingana na aliyeacha watumwa kumi, ataandikiwa thawabu mia moja, atafutiwa makosa mia moja, atakingwa na shaytwaan katika siku hiyo mpaka ifike jioni. Hakuna mtu ambaye atakuja na kitu bora zaidi kuliko alichofanya isipokuwa mtu ambaye amefanya zaidi kuliko yeye. Mwenye kusema:

سبحان الله وبحمده

“Allaah ametakasika kutokana na mapungufu na himdi zote njema ni Zake.”

mara mia katika siku, basi dhambi zake zitafutwa hata kama zingekuwa kama povu la bahari.”[4]

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Atakayesema wakati wa anaamka asubuhi na wakati wa jioni:

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَصْبَـحْتُ أَشْـهِدُك، وَأُشْـهِدُ حَمَلَـةَ عَـرْشِـك، وَمَلائِكَتِك، وَجَمـيعَ خَلْـقِك، أَنَّـكَ أَنْـتَ اللهُ لا إلهَ إلاّ أَنْـتَ وَحْـدَكَ لا شَريكَ لَـك، وَأَنَّ ُ مُحَمّـداً عَبْـدُكَ وَرَسـولُـك

”Ee Allaah! Hakika mimi nimeamka asubuhi; ninakushuhudisha na ninawashuhudia wabeba wa ‘Arshi yako na Malaika Wako, viumbe wako wote, ya kwamba Wewe ni Allaah,  hapana mungu wa haki isipokuwa Wewe, hali ya kuwa upekee yako huna mshirika, na kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wako.”

Allaah atamwokoa robo ya Moto. Atakayesema mara mbili, Allaah atamwokoa nusu ya Moto. Atakayesema mara tatu atamwokoa robo tatu ya Moto. Atakayesema mara nne, Allaah atamwokoa kabisa na Moto.”[5]

Thawbaan ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Atakayesema wakati wa jioni na anapoamka asubuhi:

رَضيتُ باللَّهِ ربًّا، وبالإسلامِ دينًا، وبِمُحمَّدٍ رسولًا

Nimeridhia Allaah kuwa Mola, Muhammad kuwa Mtume na Uislamu kuwa ndio dini yangu.”

itamthubutukia Allaah kumridhisha.”[6]

´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ambaye ataingia sokoni akasema:

لا إلهَ إلاّ اللّه وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ المُلْـكُ ولهُ الحَمْـد، يُحْيـي وَيُميـتُ  وَهُوَ حَيٌّ لا يَمُـوت، بِيَـدِهِ الْخَـيْرُ وَهوَ عَلىَ كلّ شيءٍ قَدِيرٌ

”Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, ufalme ni Wake na himdi zote njema, ambaye anahuisha na anafisha. Naye yuhai na hafi, kheri ziko mikononi Mwake; Naye juu ya kila jambo ni muweza.”

Allaah atamwandikia mema milioni moja, kufuta makosa milioni moja na kumpandisha daraja milioni moja.”[7]

34 – Kumtaja Mola (Tabaarak wa Ta´ala) daima kunaleta ulinzi dhidi ya kumsahau Yeye, jambo ambalo ni sababu ya majanga ya mja katika dunia na Aakhirah yake. Kwa kuwa kumsahau Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) humfanya mtu ajisahau nafsi yake na manufaa yake. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ نَسُوا اللَّـهَ فَأَنسَاهُمْ أَنفُسَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Na wala msiwe kama wale waliomsahau Allaah Naye akazisahaulisha nafsi zao – hao ndio mafasiki.”[8]

[1] at-Tirmidhiy (2926), aliyesema kuwa ni nzuri na ngeni. Imeungwa kwa mujibu wa Ibn Hibbaan katika “Kitaab-ul-Majruuhiyn” (1/376) na Ibn-ul-Jawziy katika “al-Mawdhwuu´aat” (3/421) na ni dhaifu kwa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (2926).

[2] at-Tirmidhiy (3462), aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri na ngeni. Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (3462).

[3] at-Tirmidhiy (3464), ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri, ngeni na Swahiyh. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (3464).

[4] al-Bukhaariy (3293 na 6403) na Muslim (2691).

[5] at-Tirmidhiy (3501), aliyesema kuwa ni nzuri na ngeni. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf-ul-Jaamiy´” (5731).

[6] at-Tirmidhiy (3389), ambaye amesema kuwa ni nzuri na ngeni. Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (3389).

[7] at-Tirmidhiy (3428), ambaye amesema kuwa ni nzuri na ngeni. Nzuri kupitia zingine kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “al-Kalim at-Twayyib” (230).

[8] 59:19

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 100-104
  • Imechapishwa: 19/08/2025