Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Na wala haitokuwa [mtu hawezi kuombea] isipokuwa baada ya idhini ya Allaah. Kama alivyosema Allaah (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anaombea mbele Yake bila ya idhini Yake?” (02:255)

Na wala Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatomwombea yeyote isipokuwa baada ya Allaah kumruhusu. Kama alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“Na wala hawamuombei uombezi yeyote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.” (21:28)

Na Yeye (Subhaanah) Haridhii isipokuwa Tawhiyd. Kama alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu, basi haitokubaliwa kwake naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (03:85)

MAELEZO

Amebainsha (Rahimahu Allaah) ya kwamba uombezi una masharti mawili:

1 – Allaah aidhinishe. Amesema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?”

2 – Allaah (´Azza wa Jall) amuwie radhi yule muombeaji na yule muombewaji. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ

“Na wala uombezi hautofaa mbele Yake isipokuwa kwa yule Aliyempa idhini.” (34:32)

وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَىٰ

“Na wala hawamuombei uombezi yeyote isipokuwa kwa yule ambaye Amemridhia.”

Ni jambo linalojulikana kuwa Allaah haridhii jengine isipokuwa Tawhiyd. Haiwezekani akaridhia kufuru. Amesema (Ta´ala):

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni Mkwasi kwenu na wala haridhii kufuru kwa waja Wake. Na mkishukuru huridhika nanyi.” (39:07)

Ikiwa mambo ni namna hii ya kwamba haridhii kufuru, ni jambo lisilowezekana akaruhusu kafiri aombewe.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 69
  • Imechapishwa: 24/11/2023