55. Kutoa pole kumependekezwa kabla na baada ya mazishi

Kutoa pole (Ta´ziyah) maana yake ni kumuamrisha yule aliyefikwa na msiba kusubiri.

´Abdullaah bin Abiy Bakr bin Muhammad bin ´Amr bin Hazm amepokea kutoka kwa baba yake ambaye na yeye alipokea kutoka kwa babu yake aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu yeyote anayempa pole nduguye wakati wa msiba isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall) atamvisha nguo ya utukufu siku ya Qiyaamah.”

Ameipokea Ibn Maajah na ni Swahiyh kwa mujibu wa Shaykh aliyesema kuwa wapokezi wake wote katika mnyororo ni waaminifu.

Maana ya kutoa pole ni kuwaliwaza wale waliofikwa na msiba, kuijaza mioyo yao, kuwatimizia haki zao na kujikurubisha kwao kwa kuwatimizia haki zao kabla na baada ya mazishi kwa kuwa wao wenyewe wameshughulishwa na msiba wao.

Imependekezwa kuwapa pole wale wafiliwa. Ni katika mambo ambayo kuna maafikiano juu yake. Sijui kama kuna yeyote aliyeenda kinyume na maoni haya isipokuwa Sufyaan ath-Thawriy aliyesema:

“Haikupendekezwa kutoa pole baada ya mazishi, kwa kuwa mambo yamekwisha.”

Maoni yenye kujulikana na yenye kutia nanga kwa wanachuoni ni kwamba imependekezwa kutoa pole kabla na baada ya mazishi kutokamana na maneno yenye kuenea ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kumpa pole aliyefikwa na msiba ana mfano wa ujira wake.”

“Hakuna muislamu yeyote anayempa pole nduguye wakati wa msiba isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall) atamvisha nduo ya utukufu siku ya Qiyaamah.”

Ni dalili inayoonyesha kuwa mapendekezo hayakufungwa.

Imependekezwa kuwapa pole wale wote waliofikwa na msiba, wazee kwa vijana, na khaswa wale wabora katika wao ili wachukuliwe kama viigizo vyema na wale wadhaifu ili wasubiri. Mwanaume asiwape pole wanawake wadogo wasiokuwa Mahaarim zake kwa kuchelea fitina. Hata hivyo inajuzu kuwapa pole wanawake waliokaa na wanaume na wengineo.

Imethibiti kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba amekataza kucheka wakati wa msiba kwa kuwa hiyo ina maana kwamba mtu anafurahishwa na msiba wa muislamu na kumvunja moyo. Wakati Imaam Ahmad alipomuona mtu anacheka wakati wa jeneza akamhama na kusema:

“Ni mafunzo gani aliyochuma huyu?”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 119-120
  • Imechapishwa: 25/10/2016