55. Du´aa wakati wa kuhisi maumivu maeneo fulani mwilini III

139 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaaa) amesimulia: “Wakati mgonjwa anapokuja au anapoletwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) husema:

اللَّهُمَّ أَذْهِبْ الْبَاسَ، رَبَّ النَّاسِ، اشْفِ وَأَنْتَ الشَّافِي، لاَ شِفَاءَ إلاَّ شِفَاؤُكَ، شِفَاءًلاَ يُغَادِرُ سَقَمًا

”Ee Allaah! Ondosha maumivu, Mola wa watu, ponyesha kwani Wewe ndiye Mponyeshaji, hakuna ponyo isipokuwa ponyo yako, ponyo isiyobakisha maradhi.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Imekuja katika tamko la Muslim:

“Akimpapasa kwa mkono wake wa kuume.”

140 –  Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba alimwambia Thaabit (Radhiya Allaahu ´anh): “Je, nisikufanyie matabano kama ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Akasema: “Ndio.” Akasema:

اللَّهُمَّ رَبِّ النَّاسِ، مُذْهِبَ البأس، اشْفِ أَنْتَ الشَّافِي، لَا شَافِيَ إِلَّا أَنْتَ، شِفَاءٌ لا يُغَادِرُ سَقَماً

”Ee Allaah, Mola wa watu, Mwenye kuondosha maumivu! Ponyesha kwani Wewe ndiye Mponyeshaji, hakuna mponyaji isipokuwa Wewe, ponyo isiyobakisha maradhi.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy.

MAELEZO

Katika Hadiyth hii kuna uwekwaji Shari´ah wa kufanya matendo na maneno kwa yule mwenye kumtembelea mgonjwa na akamfanyia matabano kwa kumuombea du´aa juu ya kupona. Kisha ampapase pale anapohisi maumivu.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

شِفَاءٌ لا يُغَادِرُ سَقَماً

”Ponyo isiyobakisha maradhi.”

Bi maana isiyobakiza maradhi baada yake.

[1] al-Bukhaariy (5675) na Muslim (2191).

[2] al-Bukhaariy (5742).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 133-134
  • Imechapishwa: 12/11/2025