54. Suala linalohusiana na ujuu wa Allaah liko wazi kabisa

Himdi zote ni za Allaah kwa sababu haki imekuwa wazi katika jambo hili kwa msaada wa hoja zenye kukata kabisa, Aayah zenye kupiga, khabari zilizopokelewa kwa mapokezi mengi na maafikiano ya Maswahabah kwa njia ya mashairi na maneno yao yaliyopokelewa, kutoka katika maneno ya wale wakuu wao na watu wao kwa jumla. Wameipokea ´Aqiydah katika jambo hilo, hali ya kuwa ni wenye kuikubali, kuiamini na kuisadikisha. Hakuna yeyote aliyewakemea. Hakuna yeyote aliyepinga. Hivo ndivyo kizazi kilivyorithiana. Maimamu wawili Abu Zur´ah na Abu Haatim wamesema:

“Haya ndio tuliwakutaemo wanachuoni wote ulimwenguni Hijaaz, ´Iraaq, Shaam na Yemen na ´Aqiydah yao ilikuwa… Allaah (´Azza wa Jall) yuko juu ya mbingu, ametengana na viumbe Wake. Hivo ndivo alivyojieleza Mwenyewe katika Kitabu Chake na kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayatakiwi kufanyiwa namna. Amekizunguka kila kitu kwa ujuzi Wake:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Hakuna aliyepingana na hayo isipokuwa mzushi aliyepindukia au mpotevu aliyetiwa katika mtihani. Mtu wa kwanza aliyepingana na hilo kutokana na vile tunavojua ni al-Jahm bin Swafwaan. Maimamu wakamkaripia na wakawakaripia wafuasi wake na wakalifanya kubwa jambo lao na Bid´ah zao.

Halafu isitoshe Jahmiyyah wanalazimika kukubaliana na waislamu pindi wanaponyanyua mikono wakati wa kuomba du´aa, wakisubiri faraja kutoka mbinguni, wakisema:

سبحان ربي الأعلى

“Ametakasika kutokamana na mapungufu, Mola wangu, uliye juu.”

na anaposoma yale yanayofahamisha hivo katika maneno ya Allaah (Ta´ala) na Sunnah za Mtume mteuliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Halafu isitoshe bado ni wenye kuendelea kusikia ´Aqiydah inayowafanya kujikuna vichwani mwao na kuzihuzunisha nyoyo zao. Siku zote wanawasikia waislamu wote kwa jumla masokoni na katika mazungumzo yao mambo yanayowafanya kughadhibika. Hawawezi wakayarudisha na wala hawawezi kuacha kuyasikiliza. Hawana juu ya Bid´ah yao hii dalili si kutoka katika Qur-aan wala Sunnah, maneno ya Swahabah yeyote au imamu mwenye kuridhiwa. Shani ya mambo ni kwamba hakuna jengine wanachofuata isipokuwa ni matamanio na kwenda kinyume na Sunnah ya mteuliwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maimamu wa uongofu.

Yule ambaye atawafikishwa na Allaah (Ta´ala) kuifuata njia iliyonyooka, kufuata uongofu wa Mtume Wake ambaye ni mkweli na mwaminifu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akawafuata Maswahabah wake watukufu na akaridhia juu ya nafsi yake yale yaliyoridhiwa na maimamu wa waislamu na waislamu wote kwa jumla, basi atakuwa ameisalimisha nafsi yake mwenyewe juu ya kwenda kinyume na waislamu hapa duniani na pia atakuwa ameisalimisha nafsi yake kutokamana na adhabu yenye kuumiza huko Aakhirah. Allaah atampa ujira mkubwa, atamwongoza katika njia iliyonyooka na atamtunuku kuwa pamoja na Mitume na waumini. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha miongoni mwa Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa pamoja na hao.”[2]

Tunamuomba Allaah (Subhaanah) atujaalie kuwa miongoni mwa wale walioongozwa katika njia iliyonyooka, kufuata yale yenye kumridhisha Mola wa walimwengu na kuiga mwongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Mtume wa mwisho na wema waliotangulia.

Hapa ndio sehemu ya mwisho. Himdi zote anastahiki Allaah pekee. Swalah na salaam zimwendee yule ambaye hakuna Mtume mwingine baada yake.

[1] 42:11

[2] 04:69

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaatu Swifat-il-´Uluww, uk. 191-192
  • Imechapishwa: 05/07/2018