Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Kunaingia pia katika yale tuliyoyataja kumuamini Allaah, Vitabu Vyake, Malaika Wake na Mitume Yake, ni pamoja na kuamini ya kwamba waumini watamuona siku ya Qiyaamah kwa macho yao kama wanavyoona jua angani lililo wazi bila ya mawingu na vilevile kama wauonavyo mwezi usiku wa mwezi mng’aro. Hawatosongamana katika kumtazama. Watamuona (Subhaanah) nao watakuwa katika uwanja wa Qiyaamah na kisha watamuona baada ya kuingia Peponi kwa namna Atakayoitaka Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

MAELEZO

Mlango huu unazungumzia waumini kumuona Mola Wao. Imeshatangulia kwa njia ya jumla ya kwamba waumini wanaamini yale yote aliyoelezea Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Pepo, Moto, Malaika, madaftari, mizani, kufanyiwa hesabu, malipo na mengineyo kuhusiana na mambo ya Aakhirah. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini yote haya kwa njia ya ujumla.

Miongoni mwa hayo vilevile kunaingia kuamini ya kwamba waumini watamuona Mola Wao siku ya Qiyaamah. Haya ni miongoni mwa maelezo kuhusu siku ya Qiyaamah ya kwamba waumini watamuona Mola Wao siku ya Qiyaamah. Amesema (Rahimahu Allaah):

“… kwa macho yao.”

kwa maana ya kwamba watamuona kwa macho yao waziwazi pasi na shaka wala shubuha yoyote:

“Hakika nyinyi mtamuona Mola Wenu kama mnavyouona mwezi usiku wa mwezi mng’aro – hamtosongamana katika kumuona. Vilevile kama mnavyoona jua wazi pasi na kuwepo mawingu.”

Hivo ndivo alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kuhusu makafiri hawatomuona. Bali watazuiawa kutokamana Naye:

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Hapana! Hakika wao siku hiyo watawekewa kizuizi [wasimuone] Mola wao.” (83:15)

Bi maana siku ya Qiyaamah.

Kuhusu waumini watamuona mara mbili:

1 – Watamuona katika uwanja muono ambao utakuwa ni maalum kwao pasi na wengineo wataokuwa wamesimama uwanjani.

2 – Watamuona namna anavyotaka (Subhaanahu wa Ta´ala) Peponi katika nyakati ambazo atawaondoshea pazia ya uso Wake mtukufu. Peponi watakuwa na nyakati maalum ambazo wanamuona. Kila mmoja atamuona katika nyakati mbalimbali kutegemea na nafasi ya kila mmoja.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 81-84
  • Imechapishwa: 16/10/2024