53. Mfungaji anatakiwa kuchunga adabu za funga


Ndugu wapendwa! Tambueni kuwa swawm inazo adabu nyingi ambazo haitimii isipokuwa kwazo na wala haikamiliki isipokuwa kwa kuzifanya. Adabu hizo zimegawanyika mafungu mawili:

1- Adabu za lazima. Ni lazima kwa mfungaji kuzichunga na kuzihifadhi.

2- Adabu zilizopendekezwa. Inatakikana kuzichunga na kuzihifadhi.

Miongoni mwa adabu za lazima ni kwamba mfungaji anatakiwa kutekeleza yale ambayo Allaah amemuwajibishia katika ´ibaadah za kimaneno na za kimatendo. Zile ambazo ni muhimu zaidi katika hizo ni swalah iliyofaradhishwa ambayo ndio nguzo ya Uislamu iliyosisitizwa zaidi baada ya shahaadah mbili. Imependeza kuichunga kwa kuihifadhi na kutekeleza nguzo zake, mambo yake ya wajibu na sharti zake. Hivyo aitekeleze ndani ya wakati wake pamoja na mkusanyiko msikitini. Hakika kufanya hivo ni katika kumcha Allaah ambako kwa ajili yake ndio imewekwa Shari´ah ya swawm na kufaradhishwa juu ya Ummah. Kuipoteza swalah ni jambo linalopingana na kumcha Allaah na kunapelekea katika kuadhibiwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ وَلَا يُظْلَمُونَ شَيْئًا

“Wakafuata baada yao waovu walipoteza swalah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu Motoni. Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akafanya mema, basi hao wataingia Pepo na wala hawatodhulumiwa chochote.”[1]

[1] 19:59-60

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 66-67
  • Imechapishwa: 16/04/2021