11 – Inamletea hali ya kurejea kwa Allaah (´Azza wa Jall). Kila anapozidi kumtaja Allaah, basi huzidi kurejea kwake kwa moyo wake katika hali zote. Matokeo Allaah humkuwa ni kimbilio lake, mahala pake pa kukimbilia na muelekeo wa moyo wake wakati wa mashaka na mitihani.

12 – Inamletea ukaribu kwa Naye. Kwa kadiri ya kumtaja kwake Allaah, huwa karibu Naye, na kwa kadiri ya kughafilika Naye huwa mbali Naye.

13 – Inamfungulia mlango mkubwa wa elimu na maarifa. Kila anapozidi Dhikr huzidi maarifa.

14 – Inamletea khofu na utukufu wa Allaah ndani ya moyo wake kwa sababu ya kushughulika na Dhikr na kuwapo kwake mbele ya Allaah (Ta´ala). Hilo ni kinyume na mwenye kughafilika ambaye heshima ya Allaah moyoni mwake ni dhaifu.

15 – Inamletea kutajwa na Allaah. Kama alivyosema (Ta´ala):

فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ

“Basi nidhukuruni na Mimi nitakukumbukeni!”[1]

Lau ingelikuwa hakuna katika Dhikr isipokuwa hii pekee, basi ingelitosha kuwa ni fadhilah na tukufu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Anayenitaja ndani ya nafsi yake, Nitamtaja katika nafsi Yangu. Anayenitaja mbele ya kundi la watu, basi Nitamkumbuka katika kundi lililo bora kuliko hilo.”[2]

16 – Inapelekea moyo kuwa na uhai. Nimemsikia Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah – Allaah aitakase roho yake – akisema:

“Dhikr ndani ya moyo ni kama maji kwa samaki. Je, samaki atakuwaje akitenganishwa na maji?”

17 – Ni chakula cha moyo na roho. Anapokikosa mja huwa kama mwili ambao umetenganishwa na chakula chake. Nilihudhuria wakati mmoja Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah akiswali Fajr, kisha akaketi akimtaja Allaah hadi karibu na nusu ya mchana. Kisha akaniambia:

“Hii ni kiamsha kinywa changu. Lau kama sintofanya hivo nguvu zangu zingedhoofika.”

Au alisema maneno yenye maana hii. Akaniambia mara nyingine maneno yenye maana kama:

“Siachi Dhikr isipokuwa kwa nia ya kupumzika ili niweze kufanya Dhikr nyingine kwa nguvu.”

18 – Inasafisha moyo kutokana na kutu yake kama ilivyotangulia katika Hadiyth. Kila chuma kina kutu. Kutu ya moyo ni kughafilika na matamanio. Usafishaji wake ni kwa Dhikr, tawbah na kuomba msamaha.

19 – Inafuta na kuyayeyusha madhambi. Kwani Dhikr ni miongoni mwa mema makubwa – na mema hufuta mabaya.

20 – Inaondoa hali ya upweke kati ya mja na Mola wake (Tabaarak wa Ta´ala). Kwani mwenye kughafilika huwa na hali ya upweke baina yake na Allaah ambayo haiondoki isipokuwa kwa Dhikr.

[1] 2:152

[2] al-Bukhaariy (7405) na Muslim (2675).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 95-96
  • Imechapishwa: 18/08/2025