52. Matabano wakati wa kuhisi maumivu na wakati wa kuumia

136 – Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna kikosi cha Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kilikuwa katika safari wakati walipotua kwenye kabila la mwarabu mmoja. Wakaomba wapokelewe kama wageni, lakini wakakataa. Mkuu wa kabila lile akawa amedungwa na nyoka. Wakajaribu kumtibu kwa kila njia, lakini haikusaidia kitu. Baadhi yao wakasema: “Nendeni kwa lile kundi lililokuja. Huenda wana kitu.” Wakaenda na kusema: “Mkuu wetu amedungwa na nyoka. Tumejaribu kumtibu kwa kila njia, lakini haikusaidia kitu. Je, kuna yeyote katika nyinyi ana chochote?” Mmoja wao akasema: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba nina tiba, lakini ninaapa kwa Allaah ya kwamba tumewaomba mtupokee kama wageni, lakini mmkakataa. Sintowatibu mpaka mtupe ujira kwa hilo.” Wakakubaliana kundi kadhaa la kondoo. Akaanza kumtemea cheche za mate na kusoma:

الْحَمْدُ للّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

“Himdi zote njema ni Zake Allaah, Mola wa walimwengu.”[1]

Mtu yule akapata uchangamfu kana kwamba ameachwa huru kutokana na hatamu. Akaanza kutembea na kutohisi maumivu yoyote. Wakawapa ujira ambao walikubaliana. Baadhi yao wakasema: “Agawanywe.” Wengine wakasema: “Msifanye chochote mpaka tufike kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika, tuangalie atatuamrisha nini.” Wakafika kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika. Akasema: “Umejuaje kuwa [Suurah hii] inatibu?” Kisha akasema: “Mmefanya jambo la sawa. Mgaweni na mnipe sehemu” na akaanza kucheka.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy.

MAELEZO

Katika Hadiyth hii kuna uwekwaji Shari´ah wa kusoma matabano kwa al-Faatihah. Jengine kuna uwekwaji Shari´ah wa kupuliza wakati wa kufanya matabano, ikiwa na maana ya kupuliza na sambamba na hilo mtu akatema mate kidogo.

[1] 01:01

[2] al-Bukhaariy (5739).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 131-132
  • Imechapishwa: 11/11/2025