Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Miongoni mwa yale tuliyotaja katika kumuamini Allaah, kunaingia pia kuamini yale aliyoelezea Allaah ndani ya Kitabu Chake, yaliyopokelewa kwa njia nyingi kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yale ambayo Salaf wa ummah wameafikiana juu yake; ya kwamba Yeye (Subhaanah) yuko juu ya mbingu Zake, juu ya ´Arshi yake na ametengana na viumbe Vyake. Naye (Subhaanah) yuko pamoja nao popote wanapokuwa na anayajua yale yote wanayoyafanya, kama Alivyoyakusanya baina ya hayo katika maneno Yake:

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاء وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

”Yeye ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ´Arshi. Anajua yanayoingia ardhini na yatokayo humo na yanayoteremka kutoka mbinguni na yanayopanda humo Naye yupamoja nanyi popote mlipo, na Allaah kwa myatendayo ni Mwenye kuyaona.” (57:04)

Kusema kwamba yupamoja nanyi popote mlipo haina maana ya kwamba amechanganyika na viumbe Vyake. Lugha haipelekei hivo. Isitoshe ni jambo linaenda kinyume na yale ambayo Salaf wa ummah wameafikiana juu yake na linakwenda kinyume na umbile ambalo Allaah amewaumba juu yake viumbe. Mwezi ni ishara katika ishara za Allaah na ni katika viumbe Vyake vidogo kabisa. Uko mbinguni daima na unakuwa pamoja na msafiri na asiyekuwa msafiri popote anapokuwa. Naye (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi, anawaona viumbe Wake, anawalinda, ana utambuzi juu yao na yasiyokuwa hayo katika maana ya uola Wake.

Maneno yote haya ambayo Allaah ameyataja – ya kwamba yuko juu ya ´Arshi na kwamba yupamoja nasi – ni haki kwa uhakika wake na wala hayahitajii makengeusho, hata hivyo lakini yanatakiwa kulindwa kutokana na dhana za uwongo kama vile kufikiria kuwa eti udhahiri wa maneno Yake:

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ

”Je, mnadhani mko katika amani na Aliyeko mbinguni… ” (67:16)

maana yake ni kwamba eti mbingu imembeba au imemfunika. Hili ni batili kwa maafikiano ya wanazuoni na watu wa imani. Kursiy ya Allaah imezienea mbingu na ardhi na Yeye ndiye anayezuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Anazizuia mbingu kwa amri Yake anafanya zisianguke kwenye ardhi kwa idhini Yake:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ

“Na miongoni mwa alama Zake ni kwamba mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake.” (30:25)

MAELEZO

Huu ni mlango muhimu zaidi ndani ya kitabu hichi na ni yenye kwenda sambamba na yale yaliyotangulia katika kitabu. Amesema (Rahimahu Allaah):

“Miongoni mwa yale tuliyotaja katika kumuamini Allaah, kunaingia pia kuamini yale aliyoelezea Allaah ndani ya Kitabu Chake, yaliyopokelewa kwa njia nyingi kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yale ambayo Salaf wa ummah wameafikiana juu yake; ya kwamba Yeye (Subhaanah) yuko juu ya mbingu Zake, juu ya ´Arshi yake na ametengana na viumbe Vyake. Naye (Subhaanah) yuko pamoja nao popote wanapokuwa na anayajua yale yote wanayoyafanya.”

Haya yamethibiti kwa dalili ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf wa ummah. Salaf wa ummah wote (Rahimahumu Allaah) ni wenye kuamini kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu ya mbingu zote, yuko juu ya ´Arshi na ametengana na viumbe Vyake. Hakuna kitu katika viumbe Vyake kilichoko kwenye dhati Yake na pia hakuna kitu katika dhati Yake kilichoko kwenye viumbe Vyake. Ametengana nao. ´Abdullaah bin al-Mubaarak na wengineo wamesema:

“Tunamtambua Mola wetu ya kwamba yuko juu ya mbingu zote, juu ya ´Arshi Yake na kwamba ametengana na viumbe Vyake. Lakini ujuzi Wake uko kila mahali.”[1]

Namna hiyo pia ndio wamesema Salaf wengine wote (Rahimahumu Allaah): kwamba Allaah (Subhaanah) yuko juu ya mbingu zote, juu ya ´Arshi na ujuzi Wake uko kila pahali. Hakuna mgongano kati ya ueneaji wa ujuzi Wake na kuwa Kwake juu. Hakika Yeye (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi na wakati huohuo ujuzi Wake uko kila mahali na umekizunguka kila kitu. Anakijua kila kitu. Ameoanisha hayo mawili katika maneno Yake (Subhaanah):

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِمَا يَكُونُ مِن نَّجْوَى ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَى مِن ذَلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Je, huoni kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo mbinguni na yale yote yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala [hauwi mnong’ono wa] chini kuliko ya hivyo, na wala wa wengi zaidi isipokuwa Yeye yupamoja nao popote watakapokuwa. kisha Atawajulisha kwa yale [yote] waliyoyatenda Siku ya Qiyaamah. Hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi daima.” (58:07)

Ameanza Aayah hii kwa kutaja ujuzi na akaimalizia kwa kutaja ujuzi. Hiyo ni dalili yenye kuonyesha kuwa ujuzi sio ujuu. Ujuzi Wake ni wenye kukizunguka kila kitu na ni jambo limethibiti kwa dalili ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf wa ummah huu. Vilevile kuwa Kwake juu ya ´Arshi ni jambo limethibiti kwa dalili ya Qur-aan na Sunnah. Hakuna mgongano kati ya hayo mawili. Hata hivyo ni jambo linalotakiwa kulindwa kutokana na dhana mbovu kama mtu kufikiria kuwa mbingu imemfunika, imembeba au kwamba ni Mwenye haja nayo. Hapana. Yeye ndiye ambaye amezisimamisha mbingu na ´Arshi. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَن تَزُولَا

“Hakika Allaah anazuia mbingu na ardhi zisitoweke.” (35:41)

وَمِنْ آيَاتِهِ أَن تَقُومَ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ بِأَمْرِهِ

“Na miongoni mwa alama Zake ni kwamba mbingu na ardhi zimesimama kwa amri Yake.” (30:25)

Viumbe vyote vimesimamishwa Naye (Jalla wa ´Alaa). Yeye ndiye Mwenye kuvizuia, Mwenye kuviendesha na Aliyeviumba. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko juu ya ´Arshi Yake na juu ya viumbe vyote.

Kuhusu Yeye kuwa pamoja na sisi na kuwa Kwake juu ya ´Arshi ni haki juu ya uhakika wake. Ni jambo lisilohitajia kupotoshwa na wala isifikiriwe kuwa amechanganyika na viumbe Vyake, kama wanavyosema Mu´tazilah, Jahmiyyah na mapote mengine yanayokanusha sifa za Allaah. Hakika (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi na ujuzi Wake uko kila mahali. Kwa msemo mwingine anakijua kila kitu kilicho mbinguni na ardhini.

Muumini anatakiwa kuamini ´Aqiydah hii kubwa iliyothibiti kwa Qur-aan na Sunnah. Hii ndio ´Aqiydah ambayo Salaf wa ummah katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waliokuja baada yao wameafikiana kwayo ya kwamba kitendo cha Allaah kuwa juu hakipingani na kuwa kwake pamoja na viumbe Vyake na kuwazunguka Kwake kiujuzi. Ujuu ni kitu kimoja na kukizunguka Kwake kila kitu kiujuzu ni kitu kingine. Hakuna chochote chenye kumpita kwenye ujuzi Wake, si mbinguni wala ardhini pamoja na kuwa yuko juu ya ´Arshi na juu ya viumbe vyote (Subhaanahu wa Ta´ala):

لِتَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ وَأَنَّ اللَّـهَ قَدْ أَحَاطَ بِكُلِّ شَيْءٍ عِلْمًا

“… ili mjue kwamba Allaah juu ya kila kitu ni Muweza na kwamba Allaah amekwishakizunguka kila kitu kwa ujuzi Wake.” (65:12)

إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi.” (08:75)

إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Hakika Allaah juu ya kila kitu ni Muweza.” (02:20)

وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقْتَدِرًا

“Na Allaah daima juu ya kila kitu ni Mwenye Uwezo wa juu kabisa.” (18:45)

[1] Ameipokea ´Abdullaah bin Ahmad katika “as-Sunnah” (44), uk. 13, ad-Daarimiy katika “ar-Radd ´alaa al-Jahmiyyah” (67), uk. 47, Ibn Battwah katika “al-Ibaanah” (2528) (02/148).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 74-76
  • Imechapishwa: 24/10/2024