Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Ambaye atazingatia nadharia hii basi ataona namna ilivyo katika upeo wa mwisho wa ujinga na upeo wa mwisho wa upotofu.Ni vipi hawa watukufu waliokuja nyuma (na khaswa wakikusudiwa wanafalsafa wa sampuli fulani) watakuwa ni watambuzi zaidi wa kitu kama hicho? Hali yao ya dini ni vurugu kusonga mbele na umbali wao kuhusu ujuzi wa Allaah ni mkubwa mno.

MAELEZO

Bi maana nadharia inayosema kuwa mfumo wa Salaf umesalimika zaidi na mfumo wa wale waliokuja nyuma ndio wenye kujua na wenye hekima zaidi. Wakati mtu mwenye akili na mwenye busara atayazingatia hayo, basi itambainikia kuwa maneno ni ya batili. Hawajui elimu ya Salaf. Kwa hivyo ni wajinga juu ya hali ya Salaf. Bali ni nadharia yenye upotofu wa hali ya juu kwa sababu inapelekea katika batili. Tukiwapa mgongo Salaf na tukasema kuwa ni wajinga na ni waghafilikaji na kwamba hawajui lolote – tutaichukua elimu yetu kutoka wapi? Kutoka kwa Jahm bin Swafwaan, Waaswil bin ´Atwaa’ na Ghazaal? Tukimwacha Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy, Maswahabah wengine waliosalia na wanafunzi wa Maswahabah, tuichukue elimu kutoka kwa Jahmiyyah, Mu´tazilah na vifaranga vyao. Huu ndio upotofu wa hali ya juu kabisa.

Wale waliokuja nyuma wana vurugu kusonga mbele kwa sababu wao wenyewe wametofautiana mno juu ya mfumo wao. ´Aqiydah yao na tafsiri zao zimetofautiana. Hawakuafikiana katika maoni bali kila mmoja ana maoni yake. Wamekanganyika. Hilo ni kwa sababu hawana marejeo sahihi ambayo ni Qur-aan na Sunnah. Qur-aan na Sunnah vinalinda dhidi ya tofauti:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

”Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.”[1]

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا

”Mkizozana juu ya jambo, basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamuamini Allaah na siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri kabisa.”[2]

Watu hawa hawarejeshi tofauti zao katika Qur-aan na Sunnah; wanazirejesha katika akili zao. Ndio maana wakatofautiana na kuwepo vurugu baina yao. Haya yanashuhudiwa na vitabu vyao, vimejaa vurugu hizi. Ni vipi watu hawa waliokuja nyuma wasiokuwa na elimu ya Qur-aan na Sunnah, ambao hawakuichukua elimu yao kutoka katika vyanzo sahihi na ambao badala yake wameichukua kutoka katika falsafa na mantiki, watakuwa bora na wajuzi zaidi kuliko Salaf? Hawaitambui dini wala hawamtambui Allaah (´Azza wa Jall), kwa sababu wamekanusha majina na sifa za Allaah? Huku ni kumjahili Allaah. Ikiwa Allaah hana usikizi, uoni, uso, mkono wala sifa yoyote – atakuwa ni kitu gani? Ametakasika Allaah kutokana na wanayoyasema. Kwa ajili hiyo wengi katika vigogo wao wamejirejea kutokana na ´Aqiydah yao. Kitendo cha kule kujirejea kwao ni ushahidi tosha juu ya kudangana na vurugu zao.

[1] 3:103

[2] 4:59

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 86-87
  • Imechapishwa: 12/08/2024