51. Mfanya uasi dhidi ya watawala ni mzushi

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Si halali kumpiga vita mtawala. Asiwepo mtu yeyote atakayemfanyia uasi. Atakayefanya hivo basi ni mtu wa Bid´ah aliye mbali na Sunnah na njia iliyonyooka.

MAELEZO

Haya yanatilia nguvu yale tuliyotaja punde ya kwamba haijuzu kwa raia kumfanyia uasi wala kumpiga vita mtawala aliyeshika udhibiti katika eneo fulani. Haijuzu kumkashifu mtawala au kueneza maasi na mapungufu yake. Badala yake inatakiwa kumnasihi kwa kumwandikia na kumpa mawaidha na kumwelekeza kwa njia inayolingana na mtawala. Ni muhimu kumnasihi. Kwa sababu Allaah akimtengeneza mtawala, basi Huwatengeneza raia kupitia kwake kwa sababu akatilia umuhimu kutengemaa kwa jamii. Licha ya kwamba kutengemaa kuko mikononi mwa Allaah, lakini mtawala ndiye sababu ya hilo. Mambo yanakuwa namna hii hata kama mtawala atakuwa dhalimu au mkandamizi. Ni lazima kwa raia kushikamana na Kitabu cha Mola wao na Sunnah za Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wavifanyie kazi mchana na usiku. Kila mmoja ataulizwa juu ya yale aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu na wala msifuate badala Yake walinzi wengine – ni machache mnayoyakumbuka.”[1]

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

”Atakayefanya hivo basi ni mtu wa Bid´ah aliye mbali na Sunnah na njia iliyonyooka.”

Ambaye atafanya uasi dhidi ya mtawala, ingawa ni kwa neno tu ambalo litachochea mkusamyiko wa watu dhidi ya watawala na kuwafanya wakumchukie, ameenda kinyume na Ahl-us-Sunnah na ameingia ndani ya Bid´ah. Bid´ah ni shari na Sunnah tupu ni kheri na rehema. Kwani Sunnah ndio njia ilionyooka ya wale walioneemeshwa katika Mitume, wakweli, mashahidi na waja wema. Tunamuomba Allaah atujaalie kuwa miongoni mwao.

[1] 07:03

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 129
  • Imechapishwa: 19/05/2026