51. Maneno ya Maswahabah kuhusu ujuu wa Allaah

55- Shaykh Abul-Husayn ´Abdul-Haqq bin ´Abdil-Khaaliq al-Yuusufiy ametukhabarisha: Muhammad bin ´Aliy bin Maymuun an-Nursiy ametuhadithia: Abu Muhammad al-Ghandajaaniy ametuhadithia: Abu Bakr bin ´Abdaan ametuhadithia: Abul-Hasan bin Sahl ametuhadithia: Muhammad bin Ismaa´iyl al-Bukhaariy ametuhadithia: Muhammad bin Fudhwayl amesema, kutoka kwa Fudhwayl bin Ghazwaan, kutoka kwa Naafiy´, kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye amesema:

“Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofariki, Abu Bakr aliinigia ndani na akambusu kwenye paji lake la uso. Akasema: “Baba na mama yangu wawe ni fidia kwako. Ni mwenye kutoa harufu nzuri katika hali ya uhai na kufa. Yule ambaye alikuwa akimuabudu Muhammad; basi atambue kuwa Muhammad amekwishakufa. Yule ambaye alikuwa akimuabudu Allaah ambaye yuko juu mbinguni; basi atambue kuwa Allaah yuhai na hafi.”[1]

56 – Muhammad ametukhabarisha: Hamd ametuhadithia: Abu Nu´aym ametuhadithia: ´Abdullaah bin Muhammad ametuhadithia: Muhammad bin Shibl ametuhadithia: Abu Bakr bin Abiy Shaybah ametuhadithia: Wakiy´ ametuhadithia, kutoka kwa Ismaa´iyl, kutoka kwa Qays aliyesema:

“Wakati ´Umar alipofika Shaam watu walimkaribisha akiwa juu ya ngamia wake na wakasema: “Ee kiongozi wa waumini! Lau ungelipanda wale farasi wa kazi, ungepokelewa na watawala na wale wakuu wao.” Akasema: “Mimi sikuoneni hapa. Amri inatoka kule” na akaashiria kwa mkono wake juu mbinguni.”[2]

57- ´Umar bin ´Abdil-Barr amesema:

“Tumepokea kutoka njia nyingi ya kwamba siku moja ´Umar bin al-Khattwaab alitoka akiwa na watu ambapo akakutana na bibi kikongwe. Akamuomba asimame ambapo akasimama. Akawa anazungumza naye naye mwanamke yule anazungumza naye. Mtu mmoja akamwambia: “Ee kiongozi wa waumini! Umewazuia watu kwa sababu ya kizee hichi?”Akasema: “Maangamivu ni yako! Unamjua huyu ni nani? Huyu ni yule mwanamke ambaye Allaah aliyasikia malalamiko yake kutoka juu ya mbingu ya saba. Huyu ni Khawlah bint Tha´labah ambaye Allaah ameshusha juu yake:

قَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّتِي تُجَادِلُكَ فِي زَوْجِهَا وَتَشْتَكِي إِلَى اللَّـهِ

“Allaah amekwishasikia kauli ya yule mwanamke anayejadiliana nawe kuhusu mumewe, na anamshitakia Allaah.”[3]

Ninaapa kwa Allaah ya kwamba lau angesimama mpaka usiku basi ningelibaki namsikiza na hakuna ambacho kingenifanya kumwacha isipokuwa swalah kisha ningelirudi kwake tena na kumsikiza.”[4]

58- Khulayd bin Ja´laj amepokea kutoka kwa Qataadah ambaye amesema:

“Siku moja ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alitoka msikitini akiwa pamoja naye al-Jaruud al-´Abdiy ambapo mwanamke mzee akasimama njiani. Akamsalimia mwanamke Yule ambapo mwanamke yule akamuitikia salamu. Mwanamke yule akasema: “Ee ´Umar! Nakumbuka wewe pindi ulipokuwa ukiitwa ”´Umayr” kwenye soko la ´Ukaadhw. Ukiwachunga watoto kwa bakora yako. Hazikupita siku nyingi mpaka ukaja kuitwa ”´Umar”, halafu ”Kiongozi wa waumini”. Mche Allaah juu ya wananchi.” al-Jaruud akasema: ”Ee mzee! Umezidisha sasa kwa kiongozi wa waumini.” Ndipo ´Umar akasema: ”Mwache.  Unamjua huyu ni nani? Huyu ni Khawlah bint Hakiym ambaye Allaah aliyasikia maneno yake kutoka juu ya mbingu ya saba. Hivyo ´Umar ana haki zaidi ya kumsikiliza.”

59 – Muhammad ametukhabarisha: Hamd ametuhadithia: Abu Nu´aym ametuhadithia: Abu Bakr Ahmad bin Muhammad bin al-Haarith ametuhadithia: al-Fadhwl bin al-Habbaab al-Jamhiy ametuhadithia: Musaddad ametuhadithia: ´Abdul-Waarith bin Sa´iyd ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin Ishaaq, kutoka kwa an-Nu´maan bin Sa´d aliyesema:

“Nilikuwa Kuufah, nyumbani kwa ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh), wakati Nawf bin ´Abdillaah alipoingia na kusema: “Ee kiongozi wa waumini! Mlangoni wamesimama mayahudi wane.”Akasema: “Njoo nao.” Waliposimama mbele yake wakamwambia: “Ee ´Aliy! Tueleze Mola wako Huyu ambaye yuko juu ya mbingu. Yukoje? Alikuweje? Alikuweje lini? Alikuwa katika kitu gani?” ´Aliy akaketi vizuri na kusema: “Enyi mayahudi! Nisikilizeni. Baada ya hapo msijishughulishe kumuuliza mwengine zaidi yangu. Mola wangu (´Azza wa Jall) ndiye wa Mwanzo. Hakuweka wazi Yeye ni kwenye kitu gani. Si mwenye kuchanganyika na kitu. Si mwenye kukita kwenye kitu. Wala si mzee mwenye kwisha.”[5]

60 – ´Abdullaah bin Muhammad ametukhabarisha: Ahmad bin ´Aliy ametuhadithia: Hibatullaah ametuhadithia: Kuuhiy bin al-Hasan ametuhadithia: Muhammad bin Haaruun al-Hadhwramiy ametuhadithia: al-Mundhir bin al-Waliyd ametuhadithia: Baba yangu amenihadithia: al-Hasan bin Abiy Ja´far ametuhadithia, kutoka kwa ´Aaswim, kutoka kwa Zirr, kutoka kwa ´Abdullaah (bin Mas´uud) (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Umbali kati ya mbingu ya mbali na Kursiy ni miaka 500. Umbali kati ya Kursiy na maji ni miaka 500. ´Arshi iko juu ya maji na Allaah yuko juu ya ´Arshi na hakuna chochote katika matendo ya wanaadamu kinachomfichikana.”

61 – Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad ametukhabarisha: Abu Bakr at-Twuraythiythiy ametuhadithia: Abul-Qaasim at-Twabariy ametuhadithia: ´Abdullaah bin Muhammad bin Ja´far ametuhadithia: ´Abdul-Ghaafir bin Salaamah ametuhadithia: Abu Thawbaan bin Mirdaad bin Jamiyl ametuhadithia: ´Abdul-Malik bin Ibraahiym al-Juddiy ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia, kutoka kwa Abu Ishaaq al-Hamadhaaniy, kutoka kwa Abu ´Ubaydah, kutoka kwa ´Abdullaah aliyesema:

“Warehemu wale walioko ardhini Atakurehemuni Yule aliyeko mbinguni.”

62 – Abu Bakr an-Naquur ametukhabarisha: Abu Bakr at-Twuraythiythiy  ametuhadithia: Abul-Qaasim at-Twabariy ametuhadithia: al-Hasan bin ´Uthmaan ametuhadithia: ´Aliy bin Muhammad bin az-Zubayr ametuhadithia: Ibraahiym bin Abiyl-´Anbas ametuhadithia: Ya´laa bin ´Ubayd ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa Abu Haashim, kutoka kwa Mujaahid aliyesema:

“Kulisemwa kuambiwa Ibn ´Abbaas kwamba kuna watu wanaopinga Qadar. Akasema: “Wanakikadhibisha Kitabu. Lau ningepata kumshika mmoja katika wao basi ningemshika kwenye maoteo ya nywele zao. Allaah (´Azza wa Jall) alikuwa juu ya ´Arshi kabla ya kuumba kitu. Ndipo akayaandika yatayokuwepo mpaka Qiyaamah kisimame. Yale yanayofanywa na watu ni mambo tayari yamekwishapangwa.”[6]

63- Abu Bakr ametukhabarisha: Abu Bakr ametuhadithia: Abul-Qaasim ametuhadithia: Ahmad bin Muhammad ametuhadithia: ´Abdullaah bin Muhammad bin Ziyaad ametuhadithia: Ibn Shayruuyah berättade ametuhadithia: Ishaaq bin Raahuuyah ametuhadithia: Ibraahiym bin al-Hakam bin Abaan ametuhadithia, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa ´Ikrimah ambaye amesema Ibn ´Abbaas amesema kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ ۖ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

“Akasema: “Basi kwa kuwa Umenihukumia kupotoka, ninaapa kwamba nitawakalia katika njia Yako iliyonyooka, kisha nitawaendea mbele yao na nyuma na kuliani kwao na kushotoni kwao; na wala hutopata wengi wao wenye kushukuru.”[7]

 “Hakuweza kusema kwamba atawaendea kwa juu yao kwa sababu alitambua kuwa Allaah yuko juu yao.”

64- ´Abdullaah bin Ahmad amepokea: Abu Bakr ametuhadithia: ´Aaswim bin ´Aliy ametuhadithia: Baba yangu ametuhadithia, kutoka kwa ´Atwaa’ bin as-Swaa-ib, kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr, kutoka kwa Ibn ´Abbaas amaye amesema:

“Fikiria kila kitu na wala usifikirie juu ya dhati ya Allaah. Kwani hakika baina ya mbingu saba mpaka kwenye Kursiy kuna nuru 7000. Naye (Tabaarak wa Ta´ala) yuko juu ya hayo.”

65 – Muhammad bin ´Abdil-Baaqiy´ ametukhabarisha: Abul-Fadhwl Hamd bin Ahmad ametuhadithia: Haafidhw Abu Nu´aym Ahmad bin ´Abdillaah bin Ishaaq ametuhadithia: Abu ´Amr bin Hamdaan ametuhadithia: al-Hasan bin Sufyaan ametuhadithia: al-Haytham bin Janaad ametuhadithia, kutoka kwa Ibn Abiy Mulaykah ambaye amesema:

“Wakati ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anh) alipokuwa katika hali ya kukata roho Ibn ´Abbaas alikuja kumtembelea. ´Aaishah akasema: “Sina haja ya kunisifu kwake.” ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Bakr akasema: “Ee mama! Ibn ´Abbaas ni miongoni mwa wana wako bora. Amekuja kukutembelea.” Akasema: “Basi mwache aingie.”Akaingia ndani na kusema: “Ee mama! Pata bishara njema! Hakuna baina yako wewe na kukutana na Muhammad na wapenzi wake isipokuwa roho kuachana na kiwiliwili chako. Ulipoteza sheni yako ya shingoni  Abwaa´ ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaanza kuitafuta. Hawakupata maji ambapo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha:

فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ

“… basi fanyeni Tayammum kwa udongo msafi na panguseni kwayo nyuso zenu na mikono yenu.”[8]

Kutokana na fadhilah zako Allaah (Ta´ala) akausahilishia Ummah huu. Halafu kukaingia mambo ya Mistwah ambapo Allaah akateremsha kukutakasa kutoka juu ya mbingu ya saba. Hakuna msikiti wowote ambapo Allaah anatajwa ndani yake isipokuwa jambo lako linasomwa usiku na mchana.”[9]

66 – Muhammad bin ´Abdil-Baqiy´ ametukhabarisha: Hamd bin Ahmad ametuhadithia: Haafidhw Abu Nu´aym Ahmad bin ´Abdillaah ametuhadithia: Abu Haamid bin Jabalah ametuhadithia: Muhammad bin Ishaaq ametuhadithia: al-Hasan bin Muhammad bin as-Swabaah ametuhadithia: ´Amr bin Muhammad al-´Anqariy ametuhadithia: ´Iysaa bin Tahmaan ametuhadithia: Nimemsikia Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) akisema:

“Zaynab alikuwa akijifakharisha juu ya wake za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Allaah aliniozesha kutoka juu mbinguni.” Kwenye harusi yake kulikuwa mikate na nyama.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“ Familia zenu ndizo zimekuozesheni na mimi nimeozeshwa na Allaah (Ta´ala) juu ya mbingu ya saba.”[10]

67 – ´Abdullaah bin Muhammad ametukhabarisha: Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy ametuhadithia: Abul-Qaasim Hibatullaah bin al-Hasan ametuhadithia: ´Ubaydullaah bin Muhammad ametuhadithia: ´Abdus-Swamad bin ´Aliy ametuhadithia: Muhammad bin ´Umar ametuhadithia: Abu Kinaanah Muhammad bin Ashras al-Answaariy ametuhadithia: Abu ´Umayr al-Hanafiy ametuhadithia, kutoka kwa Qurrah bin Khaalid, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa mama yake, kutoka kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema kuhusiana na:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ‘Arshi.”[11]

“Namna haijulikani. Kulingana ni jambo lisilokosa kutambulika. Kulikubali hilo ni imani na kulipinga ni kufuru.”[12]

[1] adh-Dhahabiy amesema:

”Imepokelewa na ad-Daarimiy  kwa cheni ya wapokezi Swahiyh na al-Bukhaariy katika ”at-Taariykh al-Kabiyr” kupitia kwa Naafiy´, kutoka kwa Ibn ´Umar.” (Kitaab-ul-´Arsh (2/159-160))

[2] adh-Dhahabiy amesema:

”Cheni ya wapokezi wake iko wazi kama jua.” (al-´Uluww, uk. 62)

al-Albaaniy amesema:

”Cheni ya wapokezi ni Swahiyh na iko juu ya masharti ya Muslim.” (Mukhtaswar-ul-´Uluww, uk. 103)

[3] 58:01

[4] adh-Dhahabiy amesema:

”Mlolongo wa wapokezi uko salama, lakini umekatika. Abu Yaziyd hakuwahi kukutana na ´Umar.” (al-´Uluww, uk. 113)

[5] adh-Dhahabiy amesema:

”Hadiyth hii ni munkati na cheni ya wapokezi wake haikuthibiti.” (al-´Uluww, uk. 65-66)

[6] al-Albaaniy amesema:

”Cheni ya wapokezi ni Swahiyh.” (Mukhtaswar-ul-´Uluww, uk. 95)

[7] 07:16-17

[8] 05:06

[9] al-Haakim (4/8-9) ambaye amesema:

”Cheni ya Hadiyth ni Swahiyh na si al-Bukhaariy wala Muslim hakuna aliyeipokea.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

[10] al-Bukhaariy (7420) na at-Tirmidhiy (3213).

[11] 20:05

[12] Ibn Taymiyyah amesema:

”Imepokelewa kutoka kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa), kutoka kwake yeye na kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo cheni ya wapokezi wake si lolote si chochote ambayo mtu anaweza kutegemea.” (Sharh Hadiyth-in-Nuzuul, uk. 34)

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaatu Swifat-il-´Uluww, uk. 148-158
  • Imechapishwa: 05/07/2018