50. Haja iliyo kubwa zaidi kuliko chakula na kinywaji

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

اهدِنَا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoze katika njia iliyonyooka… ”[1]

Yaani tuongoze, utuelekeze na ututhibitishe. Njia ni Uislamu. Imesemekana pia kuwa ni Mtume na wengine wakasema kuwa ni Qur-aan. Maana zote hizi ni haki. Iliyonyooka ni ile ambayo isiyokuwa na upindaji wowote ndani yake.

MAELEZO

Haja ya waja ya kuongozwa katika njia iliyonyooka ni juu ya kila haja na dharurah yao kwa hiyo ni juu ya kila dharurah. Haja yao hiyo ni kubwa zaidi kuliko haja yao kwa chakula na kinywaji, kwa sababu chakula na kinywaji ni sababu ya kubakia kwao katika maisha haya ya dunia. Lakini kuongozwa kwao katika njia ilionyooka ni sababu ya kufaulu kwao na furaha yao katika ulimwenguni na Aakhirah.

Kuomba kuongozwa katika njia ilionyooka kunajumuisha kuomba kuonyeshwa na kuelekezwa katika njia ya haki na uongofu. Aidha kunajumuisha kuomba kufanikishwa kuifuata njia ilionyooka. Mja kumwomba mja Mola wake katika kila Rak´ah ya Rak´ah za swalah kuongozwa katika njia ilionyooka kunakusanya kumuomba Allaah (´Azza wa Jall) amthibitishe juu ya uongofu aliokwishapata na pia kunajumuisha kuomba nyongeza ya uongofu, kama alivosema Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ

“Na wale walioongoka, basi Anawazidishia uongofu na anawapa taqwa yao.”[2]

Hakuna upingano baina ya kufasiri ”tuongoze” (اهْدِنَا) kuwa na maana ya tuonyeshe, tuongoze na tuthibitishe na baina ya kufasiri njia ilionyooka kuwa ni Uislamu, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Qur-aan; kwa sababu hiyo ni aina ya tofauti ya utofauti wa kimaelezo na siyo ya upingano. Kwa ajili hiyo Shaykh amesema:

”Maana zote hizi ni haki.”

Tafsiri za Salaf mara nyingi huwa ni za namna hii: ama tafsiri kwa maneno yenye maana zinazokaribiana zote zikiwa ni sahihi na hakuna upingano baina yake kama hapa, au tafsiri kwa mfano, nayo ni kwamba neno lenye maana pana lifasiriwe kwa baadhi ya vipengele vyake. Mfano ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

ربنا آتنا في الدنيا حسنة وفي الآخرة حسنة

“Ee Mola wetu! Tupe duniani wema na Tupe Aakhirah wema.”[3]

Kufasiri ”kheri ya dunia” (حسنة الدنيا) kwamba ni mke mwema, mtoto mwema au mali halali hakuna upingano baina yake na hiyo ni aina ya tafsiri kwa mfano.

[1] 01:06

[2] 47:16

[3] 02:201

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 56-58
  • Imechapishwa: 04/06/2026