5. Ni vipi ataswali na kutawadha mgonjwa aliyewekewa mfuko wa kukojoa?

Swali 05: Ni vipi ataswali na kutawadha mgonjwa aliyewekewa mfuko wa kukojoa?

Jibu: Atatakiwa kuswali vile hali yake ilivyo. Ni kama mfano wa mtu anayetokwa na mkojo hovyo na mwanamke anayetokwa na damu ya ugonjwa. Mgonjwa atatakiwa kuswali pale kunapoingia wakati vile hali yake ilivyo. Atafanya Tayammum ikiwa hawezi kuyatumia maji. Akiwa anaweza kuyatumia basi atalazimika kutumia maji. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[1]

Hakimdhuru kile chenye kutoka baada ya hapo. Lakini asitawadhe isipokuwa baada ya kuingia wakati. Aswali hata kama atatokwa na chenye kutoka midhali ameswali ndani ya wakati kwa sababu amelazimika kufanya hivo. Ni kama mfano wa anayetokwa na mkojo hovyo anatakiwa kuswali ndani ya wakati japokuwa mkojo unamtoka dhakarini mwake. Kadhalika mwanamke anayetokwa na damu ya ugonjwa anatakiwa kuswali ndani ya wakati japokuwa damu itatoka kwa muda mrefu. Atatakiwa kuswali vile hali yake ilivyo. Lakini kamwe asitawadhe kwa ajili ya hadathi isipokuwa pale utapoingia wakati wa swalah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia mwanamke anayetokwa na damu ya ugonjwa:

“Tawadha kunapoingia wakati wa kila swalah.”

Hivyo mtu anayetokwatokwa na mkojo, mwanamke anayetokwa na damu ya ugonjwa na huyu aliyeulizwa katika swali wanatakiwa kuswali swalah zote za faradhi na za sunnah ndani ya wakati, wasome Qur-aan kutoka ndani ya msahafu na watukufu Ka´bah kwa yule aliyeko Makkah midhali ni ndani ya wakati. Wakati ukitoka basi watajizuia mpaka watawadhe kwa ajili ya wakati ulioingia.

[1] 64:16

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Mariydhw, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 04/05/2019