Baada yake anafuata ´Umar al-Faaruuq. Ameitwa al-Faaruuq (mfarikishi) kwa sababu Allaah amefarikisha kupitia yeye baina ya haki na batili. Aliposilimu Uislamu ulitukuka kwa kuingia kwake katika Uislamu. Kabla ya Hamzah na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) waislamu walikuwa wanyonge na wakijificha katika pango la Arqam. Pindi aliposilimu Hamzah na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wakatoka nao kuelekea katika Masjid-ul-Haraam. Hapakuwepo yeyote anayewajongelea ilihali wako pamoja na Hamzah na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Hapo ndipo Allaah aliutukuza Uislamu kupitia wawili hao. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:
“Hatukuacha kuwa na nguvu na utukufu tangu aliposilimu ´Umar.”[1]
Allaah akaupa Uislamu nguvu na utukufu kupitia yeye. Ndio maana akaitwa al-Faaruuq.
Yeye ndiye khaliyfah wa pili na kadhalika ndiye Swahabah bora baada ya Abu Bakr asw-Swiddiyq kama ilivyo katika al-Bukhaariy na kwenginepo[2]. Wawili hao ndio mawaziri wawili wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bi maana wenye kumshauri Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Waziri ni mtu anayemsapoti na kumsaidia mtawala. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:
وَجَعَلْنَا مَعَهُ أَخَاهُ هَارُونَ وَزِيرًا
“… na Tukamjaalia pamoja naye – yaani Muusa – kaka yake Haaruun kuwa waziri.” (25:35)
Kwa sababu Muusa alimuomba Mola Wake na kusema:
وَاجْعَل لِّي وَزِيرًا مِّنْ أَهْلِي هَارُونَ أَخِي اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي
“Nifanyie waziri katika ahli zangu Haaruun ndugu yangu. Nitie nguvu kwaye, na umshirikishe katika jambo langu.” (20:29-32)
Hii ndio kazi ya waziri. Ni ambaye anashiriki katika maoni, anamsaidia mtawala na kumshauri na kumnasihi.
Kwa hiyo Abu Bakr na ´Umar ndio mawaziri wawili wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama ambavyo Haaruun ni waziri wa Muusa (´alayhis-Salaam).
[1] al-Bukhaariy (3863) na (3684), “al-Bidaayah wan-Nihaayah” (03/79)
[2] al-Bukhaariy (3662) na Muslim (08) na (2384).
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 117-118
- Imechapishwa: 10/01/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)