Hadiyth hii ni dalili ya kwamba ni halali kula chakula cha kafara kwa yule aliyepewa jukumu la kuitoa, ikiwa hana uwezo, na kutoa swadaqah kwa familia yake. Hili linategemea ikiwa kile kilichopewa ni kafara na si swadaqah, jambo ambalo ndio dhahiri ya Hadiyth, kama anavyosema Haafidhw, kwa sharti kwamba mtu huyo awe amepewa kama katika Hadiyth hii. Lakini ikiwa ni yeye mwenyewe ndiye kajipa nayo, basi hana ruhusa kula humo, bali anatakiwa kuwapa waliostahiki.

Maoni ya pili ya wanazuoni wengi ni kwamba kile anachokipokea si kafara, bali ni swadaqah, na kafara haidondoki kwa mtu kutokuwa na uwezo wa kuitoa, bali inabaki kuwa ni deni kwake kwa kuutmia kipimo cha kafara nyinginezo na madeni. Wamesema kwamba hakuna dalili katika Hadiyth hii inayoashiria kudondoka kwa kafara, bali dhahiri yake ni kwamba haijadondoka; kwa sababu alipomuuliza kuhusu daraja ya chini zaidi ya kafara – nayo ni kulisha chakula – na akasema: “Sina” basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinyamaza na hakumfungulia dhamana yake.

Maoni ya tatu ni kwamba kafara inadondoka endapo mtu hana uwezo wa kuitoa. Haya ndio yaliyotangaa katika madhehebu ya Imaam Ahmad na moja ya kauli mbili za ash-Shaafi´iy; kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimruhusu yule mtu kuwalisha tende watu wa nyumbani kwake. Lau kama ingekuwa bado analazimika kutoa kafara, basi isingekuwa halali kwake na hakuonyesha kwamba kafara itabaki kuwa deni kwake mpaka awe na uwezo. Na kuchelewesha ufafanuzi wa jambo katika wakati wa haja hakufai.

Maoni ya kwanza ndiyo iliyo karibu zaidi na usahihi, kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

”Chukua hiki ukatoe swadaqah kwacho.”

Kwa maana kwamba uwalishe masikini kwa niaba yako, kisha alipomueleza kuhusu ufukara wake, alimruhusu kuwapa watu wa nyumbani kwake na hakumwambia kwamba kafara ingali juu yake. Kama ingekuwa bado juu yake, basi angelimfahamisha hivyo.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/66)
  • Imechapishwa: 17/03/2025