47. Masharti yasiyo na maana katika kupangusa juu ya soksi

Kitu kinachounga mkono jambo hilo ni kwamba yale masimulizi yote yaliyopokelewa kuhusu kupaka juu ya soksi kutoka kwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayana sharti wala kizuizi. Wala hilo halifahamiki si kwa tamko lake, wala kwa maana yake, wala kwa dalili yake ya ishara. Ni wazi kwamba Maandiko hufasiriwa kutokana na ujumla wake mpaka kitapokuja chenye kufanya umaalum na yanabaki juu ya uachiliaji wake mpaka kitakapokuja chenye kuyafunga. Hapa hakukuja chenye kufanya umaalum wala chenye kuyafunga, si katika Hadiyth wala masimulizi. Hili ni mosi.

La pili tumetanguliza kwamba Imaam Abu Daawuud amepokea kutoka kwa kundi la Maswahabah kupaka juu ya soksi kwa ujumla bila sharti, kama tulivyotanguliza. Vivyo hivyo kila aliyenukuu kutoka kwa Maswahabah na wanafunzi wao (Radhiya Allaahu ´anhum) kuhusu kupangusa juu ya soksi hakunukuu kwa sharti wala kizuizi, jambo linaloonyesha kwamba kuifunga kwa sharti hakukuwa kunajulikana katika zama zao ambazo ndizo zama bora.

La tatu soksi inajulikana yenyewe katika lugha na desturi, kama tulivyonukuu maana yake kutoka kwa maimamu wa lugha na Fiqh. Hakuna yeyote aliyeweka sharti katika maana yake wala jina lake kuwa soli ya soksi iwe ya ngozi au soksi iwe nene. Ikiwa maana yake katika Fiqh na lugha ni yenye kuenea, basi hilo linahusu soksi nyembamba, nene, soksi yenye soli ya ngozi, soksi isiyo na soli ya ngozi na kadhalika – na Allaah ndiye Mjuzi zaidi.

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 20/04/2026