Alama za Bid´ah kwa wenye nazo ziko dhahiri na wazi. Alama yao iliyodhihiri na wazi zaidi ni uadui wao mkubwa dhidi ya wale watu wanaofikisha khabari za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuwadharau kwao na kuwaita kwa majina kama ya Hashwiyyah, wajinga, Dhwaahiriyyah na Mushabbihah. Kwa sababu wanaona kuwa khabari zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hazina elimu yoyote na badala yake elimu ni yale ambayo shaytwaan anawarushia kutokana na mazao ya akili zao mbovu, minong´ono ya vifua vyao vilivyo na giza, mawazo ya mioyo yao iliyokosa kheri, hoja zao bali shubuha zao zisizokuwa na maana na za batili.

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَىٰ أَبْصَارَهُمْ

”Hao ndio ambao Allaah amewalaani, akawafanya viziwi na akawapofua macho yao.”[1]

Nimemsikia al-Haakim Abu ´Abdillaah al-Haafidhw akisema: Nimemsikia Abu ´Aliy al-Husayn bin ´Aliy al-Haafidhw akisema: Nimemsikia Ja´far bin Ahmad bin Sinaan al-Waasitwiy akisema: Nimemsikia Ahmad bin Sinaan al-Qattwaan akisema:

”Duniani hakuna mtu wa Bid´ah isipokuwa anawachukia Ahl-ul-Hadiyth. Anapozua mtu, basi huondoshewa ladha ya Hadiyth moyoni mwake.”

Nimemsikia al-Haakim akisema: Nimemsikia Abul-Hasan Muhammad bin Ahmad al-Handhwaliy Baghdad akisema: Nimemsikia Muhammad bin Ismaa´iyl at-Tirmidhiy akisema:

”Nilikuwa mimi na Ahmad bin al-Hasan at-Tirmidhiy kwa imamu wa dini Abu ´Abdillaah Ahmad bin Hanbal. Ahmad bin al-Hasan akamwambia: ”Ee Abu ´Abdillaah! Walimtajia Abu Qutaylah huko Makkah Ahl-ul-Hadiyth, ambapo akasema: ”Ahl-ul-Hadiyth ni watu waovu.” Ahmad bin Hanbal akasimama, akifuta vumbi nguo zake na kusema: ”Zandiki, zandiki, zandiki”, mpaka alipoingia nyumbani kwake.”

Nimemsikia al-Haakim Abu ´Abdillaah akisema: Nimemsikia Abu Naswr Ahmad bin Sahl al-Faqiyh akisema huko Bukhaaraa: Nimemsikia Abu Naswr bin Salaam al-Faqiyh akisema:

”Hakuna kitu ambacho ni kizito kwa watu waliopinda na kinachochukiwa zaidi kwao kama kusikia Hadiyth na kuzisimulia kwa cheni zake za wapokezi.”

Nimemsikia al-Haakim akisema:

”Nimemsikia Shaykh Abu Bakr Ahmad bin Ishaaq bin Ayyuub al-Faqiyh akimuhoji bwana mmoja. Shaykh Abu Bakr akasema: ”Fulani ametuhadithia… ” Bwana yule akasema: ”Tuachie ”Ametuhadithia”. Mpaka lini ”Ametuhadithia?” Ndipo Shaykh Abu Bakr akasema: ”Simama, ee kafiri! Usiingie nyumbani kwangu baada ya leo hata siku moja.” Kisha akatugeukia na kusema: ”Sijawahi kumwambia yeyote asiingie nyumbani kwangu hata siku moja isipokuwa huyu.”

[1] 47:23

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 299-303
  • Imechapishwa: 31/12/2023