47. Aina tatu ya watu wanaowajibika kulipa Ramadhaan

Kisha wao wanagawanyika aina tatu.

1 – Wanaowajibikiwa kulipa tu bila fidia juu yao. Nao ni mgonjwa, msafiri, mjamzito na anayenyonyesha iwapo watakhofia juu ya nafsi zao.

2 – Wanaowajibikiwa fidia tu bila kulipa. Nao ni wasioweza kwa sababu ya uzee mkubwa au maradhi ambayo hayatarajiwi kupona.

3 – Wanaowajibikiwa kulipa na fidia. Nao ni mjamzito na anayenyonyesha iwapo watakhofia juu ya watoto wao tu. Fidia hapa ni kumlisha chakula masikini nusu pishi ya chakula kinacholiwa zaidi katika mji juu ya kila siku iliyompita.

Vivyo ndivyo dini yetu ilivyo ya wepesi na unafuu, inaendana na mazingira ya mwanadamu wala haimkalifishi lisilo katika uwezo wake au linalomletea mashaka makubwa yasiyovumilika. Imemuwekea katika Shari´ah mkazi hukumu zinazomfaa na msafiri hukumu zinazomfaa. Vievile imemuwekea katika Shari´ah

mwenye afya yanayomfaa na mgonjwa yanayomfaa.

Maana ya haya ni kwamba muislamu hawi mbali na ´ibaadah ya Allaah katika hali zake zote na kwamba mambo ya wajibu hayaondolewi kabisa, bali hubadilika kulingana na mazingira yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ

“… na mwabudu Mola wako mpaka ikufikie yakini.”[1]

´Iysaa (´alayhis-Salaam) amesema katika aliyoyataja Allaah kumhusu:

وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا

“… ameniusia swalah na zakaah madamu niko hai.”[2]

[1] 15:99

[2] 19:31

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 44-45
  • Imechapishwa: 18/03/2026