Maneno ya Imaam Maalik (Rahimahu Allah) yana mifano mingi ambayo imesemwa na maimamu wa Salaf na wanazuoni. Nitataja baadhi yake katika kipengele hiki. Hata hivyo ni vyema kuashiria kwamba maneno haya yaliyotangaa ya Maalik (Rahimahu Allaah) mwalimu wake Rabiy’ah ar-Ray’ amemtangulia kuyasema na inasemekena kwamba kabla ya hapo yamesemwa na mkewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Umm Salamah (Radhiya Allaahu ́alayhi ´anhaa), ingawa kupitia chanzo ambacho hakijathibiti kutoka kwake. al-Laalakaa’iy amepokea katika “Sharh Usuwl I’tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa’ah”, as-Swaabuuniy katika “´Aqiydat-us-Salaf”, Ibn Qudaamah katika “Ithbaat-ul-‘Uluww” na adh-Dhahabiy katika “al-´Uluww” – wote wamesimulia kwamba Muhammad bin al-Ashras al-Warraaq Abu Kinaanah ametuhadithia: Abul-Mughiyrah al-Hanafiy ametuhadithia: Qurrah bin Khaalid ametuhadithia, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa mama yake, kutoka kwa Ummu Salamah, ambaye amesema kuhusiana na maneno Yake (Ta’ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[1]

”Kulingana juu si kitu kisichojulikana. Namna si kitu kisichofahamika. Kuthibitisha hilo ni imani na kulikanusha ni ukafiri.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Jibu hili limepokewa kutoka kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ́anhaa), kutoka kwake na kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Hata hivyo cheni ya wapokezi wake si yenye kutegemewa.”[2]

adh-Dhahabiy amesema:

”Masimulizi haya yamehifadhiwa kutoka kwa watu kadhaa, kama vile Rabiy´ah ar-Ray’, Imaam Maalik na Abu Ja´far at-Tirmidhiy. Hata hivyo haikusihi kutoka kwa Umm Salamah, kwa sababu Abu Kinaanah si madhubuti. Vilevile simtambui Abu ´Umayr.”[3]

adh-Dhahabiy amemtaja Ibn-ul-Ashras na kusema:

”Anasimulia Hadiyth dhaifu na zenye kugongana. Si lolote.”[4]

[1] 20:05

[2] Sharh Hadiyth-in-Nuzuul, uk. 34.

[3] al-´Uluww, uk. 65.

[4] Dhayl-udh-Dhwu´afaa’ wal-Matruukiyn, uk. 58.

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 68-69
  • Imechapishwa: 05/12/2025