46. Salaf walizifasiri Aayah zinazozungumzia sifa

43 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mwenye kumwamini Allaah na Mtume Wake, akasimamisha swalah na akafunga Ramadhaan, basi inamuwajibikia Allaah kumwingiza Peponi, ni mamoja amepambana jihaad katika njia ya Allaah au amebaki katika ardhi aliyozaliwa.” Wakasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Tusiwabashirie watu jambo hilo?” Akasema: ”Hakika ndani ya Pepo kuna ngazi mia moja ambazo Allaah amewaandalia wapambanaji katika njia Yake. Umbali uliopo kati ya ngazi hizo mbili ni kama umbali uliopo kati ya mbingu na ardhi. Mkimuomba du´aa Allaah, basi mwombeni Firdaws, ambayo iko katikati na ndio Pepo ya juu kabisa. Juu yake ndio kuna ´Arshi ya Mwingi wa huruma na kutokea hapo ndio kunabubujika mito ya Peponi.”

Ameipokea al-Bukhaariy[1].

al-Bukhaariy amesema mwishoni mwa ”as-Swahiyh” yake:

”Mlango wa 22:

وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ

“… na ‘Arshi Yake ikawa juu ya maji.”[2]

وَهُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ

”Naye ni Mola wa ‘Arshi tukufu.”[3]

Kisha akasema:

”Mujaahid amesema:

”Amelingana (استوى) maana yake ni kwamba  Yuko juu (علا) ya ´Arshi.”[4]

[1] Vivyo hivyo Ahmad. Katika cheni ya wapokezi kuna makinzano niliyoyabainisha katika ”as-Swahiyhah” (921).

[2] 11:7

[3] 9:129

[4] al-Firyaabiy ameunganisha cheni ya wapokezi kwa cheni iliyo Swahiyh kutoka kwa Mujaahid. Athar hii inawaraddi waandishi wa leo ambao wanataka kuwafanya watu wafahamu kuwa eti Salaf walikuwa wanaacha kuzungumzia Aayah zinazozungumzia sifa na kwamba hawakuzifasiri kabisa, na eti walikuwa wanatosheka na kuzisoma peke yake pasi na kuzizingatia na kuzifahamu. Madai haya ameyabatilisha Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) katika vitabu vyake. Ni kweli kwamba hawakuzifasiri tafsiri zenye maana ya kushabihisha na kuzifanyia namna, bali walikemea mambo hayo kwa ukali, kama utakavyoona katika kitabu hiki kutoka kwa Maalik na wengineo. al-Laalakaa´iy amepokea kutoka kwa mwaminifu Bishr bin ´Umar (aliyefariki. 207), ambaye amesema:

”Nimewasikia wafasiri wengi wakisema kuhusu:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[4]

”Bi maana yuko juu ya ´Arshi.” (Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah (3/387-402))

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk 101
  • Imechapishwa: 24/06/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy