Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:
Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:
“Ee Alllaah! Mola wa mbingu na ardhi hizi saba! Mola wa ´Arshi tukufu! Mola Wetu na Mola wa kila kitu! Mpasuaji wa mbegu na kokwa na Ambaye umeteremsha Tawraat, Injiyl na Furqaan. Najikinga Kwako na shari ya nafsi yangu na shari ya kila kiumbe kiovu ambacho wewe una utawala juu yake. Ee Allaah! Wewe ni wa Mwanzo; hakuna kabla Yako kitu. Na Wewe ni wa Mwisho; hakuna baada Yako kitu. Na Wewe ni wa juu; hakuna juu Yako kitu. Na wewe ni wa Karibu; hakuna kinachojifichika Kwako. Nilipitie deni langu na nitajirishe na ufakiri wangu.”[1]
Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia Maswahabah pindi waliponyanyua sauti zao kwa Dhikr:
“Enyi watu! Zihurumieni nafsi zenu! Kwani hakika hamumuombi ambaye ni kiziwi wala asiyekuwepo. Hakika Yule mnayemwomba ni Mwenye kusikia Mwenye kuona na Aliye karibu. Hakika yule mnayemwomba Yuko karibu zaidi na mmoja wenu kuliko shingo ya vipando vyenu.”[2]
Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
“Hakika nyinyi mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi usiku wa mwezi mng’aro – hamtosongamana katika kumuona. Hivyo ikiwa mnaweza kuswali kabla ya jua kuchomoza na jua kuzama, basi fanyeni hivyo.”[3]
Pamoja na mfano wa Hadiyth kama hizi ambazo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasimulia kuhusu Mola wake.
MAELEZO
Mtunzi (Rahimahu Allaah) anasema kuhusu Hadiyth zingine ambazo zimetaja kuhusu sifa ikiwa ni pamoja na Hadiyth ifuatayo:
“Ee Alllaah! Mola wa mbingu na ardhi hizi saba! Mola wa ´Arshi tukufu! Mola Wetu na Mola wa kila kitu! Mpasuaji wa mbegu na kokwa na Ambaye umeteremsha Tawraat, Injiyl na Furqaan. Najikinga Kwako na shari ya nafsi yangu na shari ya kila kiumbe kiovu ambacho wewe una utawala juu yake. Ee Allaah! Wewe ni wa Mwanzo; hakuna kabla Yako kitu. Na Wewe ni wa Mwisho; hakuna baada Yako kitu. Na Wewe ni wa juu; hakuna juu Yako kitu. Na wewe ni wa Karibu; hakuna kinachojifichika Kwako. Nilipitie deni langu na nitajirishe na ufakiri wangu.”
Katika Hadiyth hii tukufu ambayo ameipokea Muslim ndani yake mna sifa aina mbalimbali:
1 – Yuko juu ya ´Arshi.
2 – Yeye ndiye Mola wa mbingu na ardhi.
3 – Mteremshaji wa Tawraat, Injiyl na Qur-aan.
Zote hizi zinajulisha ujuu Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba kutoka Kwake ndiko kunateremka kila kitu. Kutoka Kwake kunateremka maamrisho na Wahy ilihali yuko juu ya ´Arshi (Jalla wa ´Alaa) na Yuko juu ya viumbe vyote (Subhaanahu wa Ta´ala).
Vilevile mambo yote yako mikononi Mwake na anayaendesha vile anavyotaka (Subhaanahu wa Ta´ala).
Yeye ndiye wa Mwanzo na hakuna kabla Yake kitu. Yeye ni wa Mwisho na hakuna kitu baada Yake. Yeye Yuko juu na hakuna kitu juu Yake. Yeye Yuko karibu na hakuna kinachojificha Kwake. Namna hiyo ndivo imekuja ndani ya Qur-aan tukufu:
هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ
”Yeye ndiye wa Mwanzo na wa Mwisho na Aliye juu na Aliye karibu Naye kwa kila kitu ni Mjuzi.” (57:03)
Yeye ndiye wa Mwanzo na hakuna kitu kabla Yake, wa Mwisho na hakuna kitu baada yake, Yeye ni wa daima, mkamilifu na hakuacha kutokuwepo (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa msemo mwingine hakuna chochote kilichomtangulia na hafikiwi na kitu kukosekana. Yeye ni wa daima siku zote.
Yeye ni wa juu ambaye yuko juu ya viumbe vyote. Kwa msemo mwingine ni kwamba hakuna kitu kilicho juu Yake. Yeye ndiye wa juu kabisa, aliye juu ya ´Arshi Yake. ´Arshi ndio dari ya viumbe.
Yeye ni wa karibu na hakuna kinachojificha Kwake. Kwa msemo mwingine hakuna Anachohitajia na Yeye anazijua hali za waja Wake na anayajua yaliyomo ndani ya vifua vyao.
Katika du´aa hii mna njia ya kuomba kulipiwa deni na kujitosheleza na ufakiri.
[1] Muslim (2713).
[2] al-Bukhaariy (4205) na (6384) na Muslim (2704).
[3] al-Bukhaariy (554) na (574) na Muslim (633).
- Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 68
- Imechapishwa: 24/10/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)