45. Kunyanyua mikono miwili wakati wa kuomba du´aa ni jambo limesuniwa?

Swali 45: Je, kunyanyua mikono miwili wakati wa kuomba du´aa ni jambo limewekwa katika Shari´ah na khaswa wakati mtu anasafiri na ndege, gari, treni na vyombo vyenginevyo[1]?

Jibu: Kunyanyua mikono wakati wa kuomba du´aa ni miongoni mwa sababu za kuitikiwa du´aa mahali kokote. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Mola wenu ni Mwingi wa haya na Mwenye kusitiri. Anamuonea haya mja Wake anamponyanyulia mikono kuirudisha bure.”[2]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah (Ta´ala) ni mzuri na hakubali isipokuwa vilivyo vizuri. Hakika Allaah amewaamrisha waumini yale aliyowaamrisha Mitume. Akasema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَاشْكُرُوا لِلَّـهِ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ

“Enyi walioamini! Kuleni vizuri Tulivyokuruzukuni na mshukuruni Allaah mkiwa mnamwabudu Yeye pekee.”[3]

Amesema tena (Subhaanah):

يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا

“Enyi Mitume! Kuleni katika vizuri na fanyeni mema.”[4]

Kisha akamtaja mtu ambaye imerefuka safari yake, nywele zake timtim, miguu peku ambaye ananyoosha mikono yake kuelekea mbinguni akisema: “Ee Mola! Ee Mola! Chakula chake ni cha haramu, kinywaji chake ni cha haramu, mavazi yake ni ya haramu na amekulia kwa haramu – ni vipi basi atajibiwa?”[5]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Akafanya kunyanyua mikono ni miongoni mwa sababu za kuitikiwa. Pia miongoni mwa sababu za kunyimwa na kutoitikiwa ni kula haramu na kukulia kwenye haramu. Kwa hiyo ikajulisha kuwa kunyanyua mikono ni miongoni mwa sababu za kuitikiwa du´aa. Ni mamoja ndani ya ndege, treni, gari au ndani vyombo vya anga na venginevyo. Anapoomba du´aa na akanyanyua mikono yake ni miongoni mwa sababu za kuitikiwa du´aa yake. Isipokuwa katika yale maeneo ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakunyanyua mikono. Basi nasi hatutonyanyua. Mfano wa maeneo hayo ni katika Khutbah ya ijumaa. Hapa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakunyanyua mikono. Isipokuwa akiomba kuteremshiwa mvua. Hapo mtu atanyanyua mikono maeneo hapo. Vivyo hivyo kati ya sijda mbili na kabla ya kutoa salamu mwishoni mwa Tashahhud. Maeneo hayo hakuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akinyanyua mikono yake. Basi nasi hatunyanyui mikono yetu katika maeneo hayo ambayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakunyanyua mikono yake. Kwa sababu kitendo chake ni hoja kama ambavo pia kule kuacha kwake ni hoja. Hali kadhalika baada ya salamu katika zile swalah tano. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akileta zile Adhkaar zilizowekwa katika Shari´ah na hakuwa akinyanyua mikono yake. Kwa hiyo na sisi hatutonyanyua mikono yetu kwa ajili ya kumwigiliza yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu yale maeneo ambayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinyanyua mikono yake basi Sunnah ni kunyanyua mikono kwa ajili ya kumwigiliza yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jengine kufanya hivo ni miongoni mwa sababu za kuitikiwa du´aa. Vivyo hivyo kuhusu yale maeneo ambayo muislamu anamwomba Mola wake na hakukupokelewa chochote kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama alinyanyua au hakunyanyua mikono, basi sisi tutatakiwa kunyanyua kutokana na zile Hadiyth zinazofahamisha kuwa kunyanyua mikono ni miongoni mwa sababu zinazopelekea kuitikiwa du´aa kama tulivotangulia kusema.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (02/483-484).

[2] Abu Daawuud (1488).

[3] 02:172

[4] 23:51

[5] Muslim (2343).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 61-62
  • Imechapishwa: 15/05/2022