Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:
27 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:
“Wakati tulipokuwa tumekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja mtu akisema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia!” Akasema: “Una nini? Akajibu: “Nimemwingilia mke wangu ilihali nimefunga.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Unaweza kupata mtumwa ukamwacha huru?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akajibu: “Hapana.” Akasema: “Unaweza kupata chakula cha kuwalisha masikini sitini?” Akajibu: “Hapana.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanyamaza. Tulipokuwa katika hali hiyo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja na chombo kilicho na tende ambapo akauliza: “Yuko wapi muulizaji?” Akajibu: “Ni mimi hapa.” Akamwambia: “Chukua ukatoe swadaqah.” Akasema: “Hivi kuna ambaye ni fakiri kuliko mimi, ee Mtume wa Allaah? Ninaapa kwa Allaah hakuna kati ya milima miwili hii watu wa nyumba ambao ni mafukara kuliko watu wa nyumbani kwangu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka yakaonekana magego yake. Kisha akasema: “Walishe watu wa nyumbani kwako.”[1]
Wameipokea wasaba. Tamko ni la Muslim.
MAELEZO
Hadiyth hii ni dalili ya ukubwa wa dhambi ya kujamiiana kwa mfungaji wakati wa mchana wa Ramadhaan, kutokana na maneno ya yule bwana: “Nimeangamia.” Vilevile na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Na nini kilichokuangamiza?” Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkubalia kwamba kitendo chake hicho ni cha kuangamiza. Lau kama isingekuwa hivyo, basi angelirahisisha jambo hilo. Imekuja katika Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwamba alisema:
“Nimeungua.”[2]
Na huyu mtu alikuwa mjinga wa kile kinachompasa afanye, lakini si mjinga wa kwamba kujamiiana ndani ya Ramadhaan ni haramu, kwa sababu hii ndio maana alisema: “Nimeangamia.”
[1] al-Bukhaariy (1936) na Muslim (1111).
[2] al-Bukhaariy (1953) na Muslim (1112).
- Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/63-65)
- Imechapishwa: 26/02/2025
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)