45. Allaah anakuwa kwako vile unavyokuwa kwa wengine

Imekuja katika Hadiyth Swahiyh inayosema:

“Hakika Allaah anapenda witiri.”[1]

Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Mwingi wa rehema na anawapenda wenye huruma. Anamrehemu miongoni mwa waja Wake yule anayekuwa na huruma. Naye ni Mwenye kusitiri na anampenda yule anayewasitiri waja Wake. Naye ni Mwingi wa kusamehe na anampenda yule anayewasamehe wengine. Naye ni Mwingi wa msamaha na anawapenda wale wanaowasamehe wengine. Naye ni Mpole na anawapenda wale wanaowafanyia upole wengine. Naye anachukia mkali, mgumu, mwenye moyo mgumu, mwenye jeuri na kiburi. Naye ni Mpole na anapenda wenye kufanya upole. Ni Mvumilivu na anapenda uvumilivu. Ni Mwenye kufanya wema na anapenda wema na watu wema. Ni Mwadilifu na anapenda uadilifu. Naye ni Mkubali wa udhuru na anampenda anayekubali udhuru wa wengine. Anamlipa mja Wake kwa mujibu wa sifa hizi kwa mujibu wa kile alichonacho na kile asichokuwa nacho. Basi anayesamehe, husamehewa. Anayeghufuria, hughufuriwa. Anayesamehe watu, husamehewa. Anayemuonea huruma kiumbe, huonewa huruma. Anayewafanyia wema viumbe, hufanyiwa wema. Anayetowa kwao, hutolewa kwake. Anayewanufaisha, hunufaika. Anayewasitiri, husitiriwa. Anayewachukulia kwa upole, huchukuliwa kwa upole. Anayewafuata aibu zao, hufuatwa aibu yake. Anayewafedhehi, hufedheheshwa. Anayewazuilia kheri, huzuiliwa kheri. Anayewatesa, Allaah humtesa. Anayewatendea hila, hutendewe hila. Anayedanganya, hudanganywa. Anayewatendea waja kwa sifa fulani, Allaah humtendea kwa sifa hiyohiyo duniani na Aakhirah. Allaah (Ta´ala) anakuwa kwa mja Wake vile ambavyo mja anakuwa kwa waja Wake.  Hii ndiyo maana ya Hadiyth:

“Anayemsitiri muislamu, basi Allaah humsitiri duniani na Aakhirah. Anayempunguzia muumini dhiki miongoni mwa dhiki za dunia, basi Allaah humpunguzia dhiki miongoni mwa dhiki za siku ya Qiyaamah. Anayemrahisishia mwenye dhiki, basi Allaah humrahisishia hesabu yake. Anayemsamehe mwenye kujuta, basi Allaah humsamehe makosa yake. Anayempa muda mwenye dhiki au akafuta deni lake, basi Allaah humweka chini kivuli cha ´Arshi Yake.”[2]

Hii ni kwa sababu yeye amempa kivuli cha subira na msamaha, akamuokoa na joto la madai, na shida ya kulipa kwa ugumu wa hali, basi ndipo Allaah atamuepusha na joto la jua siku ya Qiyaamah na kumweka chini kivuli cha ´Arshi Yake.

[1] al-Bukhaariy (6410) na Muslim (2677).

[2] Muslim (2699).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 80-81
  • Imechapishwa: 13/08/2025