Tambua kwamba Allaah (´Azza wa Jall), ambaye ndiye mkweli wa wazungumzaji, ya kwamba kiti cha enzi cha Balqiys kilikuwa kikubwa:

وَلَهَا عَرْشٌ عَظِيمٌ

“… na anacho kiti cha ufalme kikubwa.”[1]

Bi maana kiti cha enzi kikubwa kuhusiana naye. Hata hivyo hatuna utambuzi wa kina kuhusu kiti chake cha enzi, kiwango chake wala maumbile yake. Mmoja katika raia wa Sulaymaan (´alayhis-Salaam) alimletea nacho na kukiweka mbele yake kabla ya kuwahi kupepesa jicho lake. Kutakasika kutokana na mapungufu ni kwa Allaah Aliyetukuka. Hakuna anayepinga karama za mawalii isipokuwa mjinga tu. Je, kuna karama iliyo juu ya hii? Inasemekana kuwa aliomba du´aa kwa jina kuu zaidi la Allaah, ambapo akatokea Yemen kwenda Shaam kwa muda wa kupepesa macho. Hakuna jengine isipokuwa imani safi na kusadikisha. Hapa hakuna nafasi ya kuingiza akili. Bali tunaamini na kusadikisha. Hili linahusiana na jambo dogo alilolifanya mwanadamu. Aliweza kukileta kwa umbali huu mkubwa kwa idhini ya Allaah. Unafkiria nini juu ya vile vitanda na majumba ambayo Allaah (Ta´ala) amewaandalia waja Peponi? Vitanda, ambavyo urefu na upana wake ni sawa na mwendo usiopungua mwezi mzima, vilivyotengenezwa kwa lulu nyeupe au rubi nyekundu, ambapo kila kinachouzwa katika hayo ni bora kuliko ufalme wa dunia nzima:

فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ

“Amebarikika Allaah mbora wa wenye kuumba.”[2]

Naapa kwa Allaah! Tunaamini mambo yaliyofichikana na tunayakinisha maelezo ya mkweli. Katika Pepo kuna ambavyo macho haijaviona, masikio hayajavisikia wala hayajapitika ndani ya moyo wa mwanadamu. Unafikiriaje kuhusu ukubwa wa ´Arshi ya Aliye juu na Mkubwa kabisa ambayo amejifanyia Mwenyewe inapokuja katika kunyanyuka kwake, upana wake, nguzo zake, dutu, wabebaji wake, uzuri wake na hadhi yake? Imepokelewa kwamba inatokana na rubi nyekundu. Pengine umbali wake ni sawa na miaka 500.000[3]. Hakuna mwabudiwa wa haki mwingine asiyekuwa Allaah, Mpole, Mkarimu. Hakuna mwabudiwa wa haki mwingine asiyekuwa Allaah, Mola wa ´Arshi tukufu. Hakuna mwabudiwa wa haki mwingine asiyekuwa Allaah, Mola wa mbingu saba na Mola wa ´Arshi tukufu. Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Allaah ametakasika na mapungufu sawa na idadi ya viumbe Wake. Allaah ametakasika na mapungufu kwa radhi Yake. Allaah ametakasika na mapungufu kwa uzito wa ´Arshi Yake. Allaah ametakasika na mapungufu kwa wino wa maneno Yake. Haiwezekani hata kama kuelezea baadhi ya viumbe – na Allaah yujuu na ni mkubwa zaidi:

فَلَمَّا أَحَسَّ عِيسَىٰ مِنْهُمُ الْكُفْرَ قَالَ مَنْ أَنصَارِي إِلَى اللَّـهِ ۖ قَالَ الْحَوَارِيُّونَ نَحْنُ أَنصَارُ اللَّـهِ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَاشْهَدْ بِأَنَّا مُسْلِمُونَ

“Basi pindi ‘Iysaa alipohisi kutoka kwao ukafiri [kwa kumuamini], alisema: “Nani watanisaidia [kulingania] katika njia ya Allaah? Wakasema wafuasi watiifu: “Sisi ni wasaidizi wa Allaah! Tumemwamini Allaah; na shuhudia ya kwamba sisi tumejisalimisha kwa Allaah!”[4]

Maangamivu kwa akili zinazopekua, nyoyo zinazokanusha na nafsi zinazokanusha! Hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria na hali ardhi yote itakamatwa mkononi Mwake siku ya Qiyaamah na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kulia. Ametakasika kutokana na mapungufu, ametukuka kutokamana na yale wanayomshirikisha! Ee Allaah! Kwa haki Yako juu yako, kwa jina Lako tukufu zaidi na kwa maneno Yako kamili; ithibitishe imani ndani ya nyoyo zetu na utufanye ni waongofu na wenye kuongoza. Mbingu saba ukizilinganisha na Kursiy si kitu isipokuwa ni kama mfano wa kijipete cha chuma kilichotupwa katika uwanja mkubwa, na ´Arshi ukiilinganisha na Kursiy ni kama huo uwanja mkubwa ukiulinganisha na kijipete hicho[5]. Sikiliza na utie akilini na uzingatie yale unayoambiwa. Kimbilia katika kuamini yaliyofichikana. Kwani kupewa khabari si kama kushuhudia kwa macho. Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ

“Wale wanaobeba ‘Arshi na walioizunguka wanasabihi kwa himidi za Mola wao na wanamwamini na wanawaombea msamaha wale walioamini [kwa madhambi yao]: “Mola wetu, rehema na elimu [Yako] imekieneza kila kitu! Hivyo basi, wasamehe wale waliotubu na wakafuata njia Yako, na wakinge na adhabu ya Moto.”[6]

وَتَرَى الْمَلَائِكَةَ حَافِّينَ مِنْ حَوْلِ الْعَرْشِ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ

”Utawaona Malaika wakizunguka pembezoni mwa ‘Arshi wanatukuza kwa himdi za Mola wao.”[7]

وَالْمَلَكُ عَلَىٰ أَرْجَائِهَا ۚ وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ يَوْمَئِذٍ تُعْرَضُونَ لَا تَخْفَىٰ مِنكُمْ خَافِيَةٌ

”… na Malaika watakuwa kandoni mwake na watabeba ‘Arshi ya Mola wako juu yao siku hiyo [Malaika] wanane. Siku hiyo mtahudhurishwa; halitofichika tendo lenu lolote lile la siri.”[8]

رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ ذُو الْعَرْشِ

”Mola, Mwenye ujuu wa vyeo na daraja.”[9]

Qur-aan imesheheni kutaja ´Arshi na vivyo hivyo Athaar. Kutokana na hilo ´Arshi haiwezi kabisa ikawa na maana ya ufalme. Acha kiburi na mabishano, kwa sababu mabishano juu ya Qur-aan ni ukafiri. Sio mimi niliyeyasema, isipokuwa ni mteule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[10].

[1] 27:23

[2] 23:14

[3] Tunaiamini ´Arshi ya Mwingi wa huruma (Tabaarak wa Ta´ala), lakini tunaieleza kutokana na ilivyothibiti ndani ya Qur-aan na Sunnah peke yake. Ingelikuwa vizuri endapo mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) angelazimiana na hilo na akaacha kuieleza kwa kudhania na kubahatisha, khaswa kwa kuzingatia kwamba ametaja katika ile ya asili kwamba Wahb bin Munabbih amesema:

”´Arshi ni umbali wa miaka 50.000.”

Alisema 50.000 na hakusema 500.000. Kwa hali yoyote ni katika khabari za wana wa israaiyl ambazo hakuna faida yoyote kuzitaja isipokuwa kwa lengo la kuzindua. Kwa ajili hiyo nimeyaondosha katika toleo hili fupi.

[4] 3:52

[5] Anaashiria Hadiyth niliyoihakiki katika “Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (109) na ambayo itakuja huko mbele kwenye kitabu.

[6] 40:7

[7] 39:75

[8] 69:17-18

[9] 40:15

[10] Kwa haki kabisa mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amethibitisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema namna hiyo. Ni jambo limesihi na kuthibiti kupitia njia nyingi. Maimamu wengi wameisahihisha kama tulivyotangulia kuashiria hilo.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk 99-101
  • Imechapishwa: 24/06/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy