44. Du´aa wakati wa majanga na kuhisi dhiki

127 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema wakati wa janga

لا إِله إِلاَّ اللهُ الْعَظِيمُ الْحَلِيمُ لاَ إِله إِلاَّ الله رَبُّ الْعَرْشِ العظيم لاَ إِلهَ إِلاَّ الله ربُّ السَّمواتِ وَرَبُّ الأَرض وَرَبُّ العرش الْكَرِيم

“Hakuna mwabudiwa  wa haki isipokuwa Allaah, aliye Mtukufu Mpole. Hakuna mwabudiwa  wa haki isipokuwa Allaah, Mola wa ´Arshiy tukufu. Hakuna mwabudiwa  wa haki isipokuwa Allaah, Mola wa mbingu, Mola wa ardhi na Mola wa ´Arshiy tukufu.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Imekuja katika upokezi wa al-Bukhaariy:

لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ الْعَظِيمُ الْحَلِيمُ، لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ رَبُّ السَّمَوَاتِ وَالْأَرْضِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ

“Hakuna mwabudiwa  wa haki isipokuwa Allaah, aliye Mtukufu Mpole. Hakuna mwabudiwa  wa haki isipokuwa Allaah, Mola wa mbingu na ardhi na Mola wa ´Arshiy tukufu.”[2]

Imekuja katika upokezi wa Muslim:

“Ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapofikwa na dhiki husema hivo.”

MAELEZO

Hii ni du´aa tukufu ambayo imewekwa katika Shari´ah kuisema wakati wa janga na dhiki. Ni du´aa ya ´ibaadah (دعاء العبادة) ambayo ndani yake imekusanya du´aa ya maombi (ودعاء المسألة). Ni vyema pia ikiwa ataomba baada yake na kumwomba Allaah mahitajio yake ili awe amekusanya kati ya du´aa ya ´ibaadah na du´aa ya maombi.

Imeitwa “du´aa”ingawa ni Dhikr na sifa, kwa sababu mwombaji na anayemsifu Allaah ameomba kimaana, kwa sababu anatafuta thawabu. Na yule anayeomba moja kwa moja ameomba kimatamshi.

[1] al-Bukhaariy (6346) na Muslim (2730).

[2] al-Bukhaariy (6345).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 127
  • Imechapishwa: 09/11/2025