43. Watu wa misimamo mikali sio Salafiyyuun

Wanasema kuwa njia ya Salaf imesalimika zaidi kwa sababu hawakuingia katika kufasiri na kutafiti, walichofanya ni kunyamaza. Wamefikiria kuwa Salaf walikuwa wenye kuyaamini matamshi peke yake na hawakuwa wakijua maana yake. Kwa ajili hiyo ndio maana wakasalimika na makosa. Kuhusu wale waliokuja nyuma, waliingia katika upambanuzi, wakayatafiti mambo na hivyo wakafikia katika elimu ambayo haikuwa inatambulika kwa Salaf. Kwa ajili hiyo wao wakawa ni wajuzi na wenye hekima zaidi kuliko Salaf. Bi maana yenye ustadi na imara zaidi.

Maneno haya ni batili. Hapana shaka kwamba Salaf ndio ambao wametilia umuhimu na kuyafahamu maandiko. Wao ndio wanarejelewa katika kuifahamu Qur-aan na Sunnah. Hawarejelewi wale waliokuja nyuma katika mambo hayo. Mzuri katika wale waliokuja nyuma ni yule ambaye ameenda sambamba na Salaf na akafuata mfumo wao. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[1]

Wamewafuata katika elimu, ´ibaadah, ´Aqiydah, maneno na matendo. Wamewafuata kwa wema, bi maana kuiimairi njia yao. Hawakuchupa na kupindukia mipaka wala hawakuzembea na kuchukulia wepesi. Wamewafata kati na kati na unyookaji, pasi na kuchupa mpaka na kuzembea.

Wako wanaodai kuwa wanawafata Salaf lakini wanaenda kinyume nao, wanachupa mpaka na kuzidisha. Hivyo wanatoka nje ya njia ya Salaf.

Wako watu wengine ambao wanadai kuwa wanawafata Salaf lakini wanachukulia wepesi na kufanya ulegevu na wanatosheka na kule kujinasibisha.

Yule anayewafuata Salaf anakuwa kati na kati na ananyooka kati ya kuchupa mpaka na kuzembea. Hakuna uchupaji mipaka wala kuchukulia wepesi. Hii ndio njia ya Salaf, na si yale yanayotokea kwa baadhi ya wajinga ambao wanajiita Salafiyyuun kisha wanaenda kinyume na Salaf, wanakuwa na ususuwavu na kuwakufurisha watu pasi na haki, wanawatia watu katika ufuska, wanawatia watu katika Bid´ah pasi na vigezo vinavyokubalika katika Shari´ah. Salaf hawakuwa wanafanya hivo. Salaf hawakuwa wakiwatia watu katika Bid´ah, wakikufurisha au kuwatia watu katika ufuska isipokuwa kwa dalili kutoka katika Qur-aan. Watu hawa wanafanya hivo kwa matamanio na ujinga. Ukitaka kuwa Salafiy wa kikweli basi unalazimika kuisoma ´Aqiydah ya Salaf na uimairi na uitambue kwa utambuzi. Baada ya hapo ndio uitendee kazi pasi na kuchupa mipaka wala kuzembea. Huu ndio mwenendo wa Salaf. Ama madai peke yake na kujinasibisha pasi na uhalisia ni jambo linalodhuru na wala halinufaishi kitu.

[1] 09:100

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 75-77
  • Imechapishwa: 06/08/2024