Ni wapumbavu mno wanaosema kuwa njia ya Salaf ni salama zaidi lakini njia ya wale waliokuja nyuma ndio yenye kujua na yenye hekima zaidi. Huku ni kujigonga. Salama haipatikani pasi na elimu. Hakuna salama inayokuwa na ujinga. Isitoshe inawezekanaje wale waliokuja nyuma wakawa ni wajuzi zaidi kuliko Salaf ambao wamejifunza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoka kwa Maswahabah? Je, hili linawezekana kweli kuwa zile karne zilizokuja nyuma zikawa zinajua zaidi kuliko Salaf? ´Imraan bin Husayn (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Bora ya ummah ni karne yangu. Kisha wale watakaofuata. Kisha wale watakaofuata. Baada ya hapo watajitokeza watu ambao watashuhudia pasi na kuombwa kutoa ushuhuda na watatoa kiapo pasi na kukitekeleza. Kutadhihiri kati yao unene.”

´Imraan amesema:

”Sijui baada ya karne yake alitaja karne mbili au tatu.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametoa khabari kuhusu hawa watakaokuja nyuma na akaeleza kuwa watasheheni matamanio, ujinga, uwongo na mengi mengine. Watu hawa wanasema kinyume na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanasema kuwa waliokuja nyuma wana hekima na ni wajuzi zaidi kuliko Salaf. Anayesema hivo hakumtambua Allaah (´Azza wa Jall) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ipasavyo. Ndio maana amefanya ujasiri huu wa kipumbavu na akafikiria namna hii. Hawajui ni kina nani Salaf. Ndio maana amefanya ujasiri huu wa kipumbavu na akasema maneno haya mabaya.

[1] al-Bukhaariy (2651) na Muslim (2535).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 74-75
  • Imechapishwa: 06/08/2024