43. Kila mtu anampenda mkarimu, kila mtu anamchukia mbakhili

Mtu mkarimu huwa karibu na Allaah (Ta´ala), karibu na viumbe Wake, karibu na familia yake, karibu na Pepo na mbali na Moto. Mbakhili huwa mbali na viumbe wa Allaah, mbali na Pepo na karibu na Moto. Ukarimu wa mtu humfanya apendwe hata na maadui zake, lakini ubakhili wake humfanya achukiwe hata na watoto wake. Kama inavyosemwa:

Huonekana aibu ya mtu kwa watu kwa ubakhili wake

na huificha aibu hiyo kwao wote kwa ukarimu wake

Jivike nguo za ukarimu, kwani mimi

naona kila aibu hufunikwa na ukarimu

Ambatana na mtu huru unapotaka kuambatana,

kwani anayempamba au kumshusha kijana ni wenzake

Punguza maneno yako kadiri uwezavyo,

kwa kuwa maneno yanapopungua, basi makosa hupungua

Mali ya mtu inavyopungua ndivyo marafiki hupungua

na ardhi na anga huwa finyu kwake

Anakuwa hajui, hata kama ana busara

Je, asonge mbele au arejee nyuma

Mtu asipochagua rafiki mwema kwa nafsi yake

basi watangazie watu: ”Hayo ndio malipo yake!”

Maana ya ukarimu ni kutoa kile mtu anachokihitaji wakati wa uhitaji, kwa namna ya kukifikisha kwa mwenye kustahiki kwa kadri ya uwezo wake. Si sahihi kusema, kama walivyodai baadhi ya watu waliopungukiwa matendo, kwamba ukarimu ni kutoa tu kile kilichopo hata kama mtu hakihitaji. Lau ingelikuwa hivyo, basi jina la israfu na ubadhirifu lingeondoka, wakati ambapo Qur-aan imekataza wazi tabia hizo na Sunnah pia imekataza.

Kwa hiyo ikiwa ukarimu ni sifa njema, basi anayezingatia mipaka yake huitwa karimu na anastahiki kusifiwa. Lakini anayepungukiwa huitwa mbakhili na anastahiki kusimangwa. Kuna masimulizi yanayosema:

“Hakika Allaah (´Azza wa Jall) ameapa kwa utukufu Wake kwamba hatomfanya mbakhili kuishi karibu Naye.”[1]

[1] Tazama “adh-Dhwa´iyfah” (1284-1285).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 76-77
  • Imechapishwa: 13/08/2025