Kisha wanazuoni wametofautiana ni kipi kilicho bora katika safari kufunga au kula? Abu Haniyfah na ash-Shaafi´iy na Ibn Hajar ameinasibisha kauli hii kwa wanazuoni wengi – ya kwamba kufunga ndio bora ikiwa hakuna uzito wala madhara yoyote. Aidha hiyo ndiyo ilikuwa desturi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ilivyo katika Hadiyth ya Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo yeye alifunga (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Abdullaah bin Rawaahah (Radhiya Allaahu ´anh)[1]. Isitoshe kufunga ni kufanya haraka katika kuondosha deni la ´ibaadah na ni rahisi zaidi ikiwa atafunga huku watu wote wakiwa wamefunga. Ibn Hajar ameyapa nguvu maoni haya. Imaam Ahmad na wenzake wameona kuwa kula ni bora hata kama hapatakuwa na ugumu wowote. Dalili yao ni Hadiyth ya mlango huu, kwani maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ni ruhusa kutoka kwa Allaah. Yule mwenye kuitendea kazi amefanya vizuri.”

inathibitisha kuwa kula ni bora, kwa sababu Allaah anapenda ruhusa Zake zitumike. Aidha amesema kuhusu swawm:

“Na yeyote anayependa kufunga, basi hakuna dhambi juu yake.”

Mtazamo wa tatu ni kuwa kilicho bora ni kilicho rahisi zaidi, basi mwenye kuona kufungua kuwa rahisi zaidi kwake, basi hicho ndicho bora kwake, na mwenye kuona kufunga kuwa rahisi zaidi kwake, basi hicho ndicho bora. Haya ni maoni ya ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz, Mujaahid na Qataadah na yamechaguliwa na Ibn-ul-Mundhir[2]. Maoni haya ya mwisho ni yenye nguvu na yanakusanya dalili nyingi kuhusu mada ya swawm katika safari na inayafanyia kazi yote.

Fahamu kuwa hakuna tofauti katika uhalali wa kula safarini kati ya safari ndefu au fupi, wala kati ya safari iliyozuka kwa ajili ya jambo fulani au ya daima kama vile madereva wa ndege na teksi, kwa sababu ya kuenea kwa dalili. Isitoshe ruhusa ya kula imefungamanishwa na safari; kwa kuwa safari ni sehemu yenye ugumu. Kwa hiyo haishurutishwi kuwepo kwa ugumu. Ikiwa kwa mfano atasafiri kwa ndege, basi ana ruhusa ya kufungua kwa sababu yeye ni msafiri aliyeliacha mji wake – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

[1] al-Bukhaariy (1945) na Muslim (1122).

[2] al-Ishraaf (04/143).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Minhat-ul-´Allaam fiy Sharh Buluugh-il-Maraam (05/59-60)
  • Imechapishwa: 26/02/2025