42. Tuna matarajio kwa watenda mema na tunakhofia kwa watenda madhambi

Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

70 – Tunataraji wafanyao wema miongoni mwa waumini atawasamehe na kuwaingiza Peponi kwa rehema Zake. Hatujiaminishi nao na wala hatuwashuhudii kuingia Peponi.

MAELEZO

Shaykh Ibn Maaniy´ (Rahimahu Allaah) amesema:

”Tambua kuwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah hawamshuhudii muislamu yeyote anayekufa kuingia Peponi au Motoni muda wa kuwa hajashuhudiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo wana matarajio kwa yule mtenda mema na wanachelea juu ya mtenda dhambi. Kwa ajili hiyo utaona kosa linalofanywa na watu wengi pale wanapomtaja mwanachuoni, kiongozi, mfalme au mwengine kwamba amesamehewa au ameingia Peponi. Lililo baya zaidi kuliko hayo ni pale wanapothibitisha kuwa ameenda katika waja walio katika daraja za juu kabisa. Hapana shaka kwamba huku ni kuzungumza juu ya Allaah bila ya elimu, jambo ambalo linalingana na shirki. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika si vyenginevyo Mola wangu ameharamisha machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [aina zote] na ukandamizaji bila ya haki na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa ambayo hakukiteremshia mamlaka na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[1]

Kuhusu mshirikina, tunashuhudia kuwa ameingia Motoni kwa sababu Allaah amesema:

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah, basi hakika Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni Motoni.”[2][3]

[1] 7:33

[2] 05:72

[3] Haashiyah ´alaa al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 56-57

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 02/10/2024