33- Baada ya kumaliza kumuosha maiti ni lazima kumvika sanda. Kutokana na amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya jambo hilo katika Hadiyth ya Muhrim ambaye alivunjwa shingo yake na ngamia wake:

“… na mumkafini… “

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika kipengele cha 3 nambari. 8 ukurasa wa 12-13

34- Sanda au thamani yake itokamane na mali ya maiti ijapokuwa hakuacha nyingine zaidi ya hiyo. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya Khabbaab bin al-Aratt ambaye ameeleza:

“Tulihajiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika njia ya Allaah tukitafuta uso wa Allaah ambapo ikawajibika ujira wetu kwa Allaah. Miongoni mwetu ambao wamekwishakupita hawakula chochote kutoka katika ujira wao. Mmoja wa watu hao ni Musw´ab bin ´Umayr ambaye aliuawa siku ya Uhud na hakujapatikana kwake chochote [katika upokezi mwingine imekuja: “Hakuacha] isipokuwa nguo moja tu. Tulikuwa tunapoiweka kichwani mwake basi miguu yake inabaki wazi na tunapoiweka miguu mwake basi kichwa chake kinabaki wazi. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Iwekeni katika ile sehemu kuanzia kichwa chake [Katika upokezi mwingine imekuja: “Mfunikeni kwayo kichwa chake] na wekeni juu ya miguu yake majani ya al-Idhkhira[1]. Miongoni mwetu wako wale ambao matunda yao yalikuwa yamekwishawiza na wako tayari kuyavuna.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/110), Muslim (03/45) na mtiririko ni wake, Ibn Jaaruud katika “al-Muntaqaa” (260), at-Tirmidhiy (357) ambaye ameisahihisha, an-Nasaa´iy (01/269), al-Bayhaqiy (03/401), Ahmad (06/695) na upokezi wa pili ni wake na wa at-Tirmidhiy.

Abu Daawuud amepokea kutoka kwake (02/14,62) maneno yake kuhusu Musw´ab:

“Aliuawa siku ya Uhud… ”

Upokezi wa tatu ni wake. Katika maudhui haya zipo Hadiyth kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf ambazo zimepokelewa na al-Bukhaariy na wengineo.

35- Sanda inatakiwa iwe refu na yenye kumwenea inayofunika mwili wake mzima. Hayo ni kutokana na Hadiyth ya Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoa Khutbah ambapo akamtaja bwana mmoja katika Maswahabah zake ambaye aliuawa na akavikwa sanda isiyokuwa refu na akazikwa usiku. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akagombeza mtu kuzikwa wakati wa usiku mpaka kwanza aswaliwe. Isipokuwa pale ambapo mtu atalazima kufanya hivo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Pindi mmoja wenu atapomzika nduguye basi aifanye vizuri ile sanda yake [akiweza].”

Ameipokea Muslim (03/50), Ibn Jaaruud (268), Abu Daawuud (02/62), Ahmad (03/295, 329). at-Tirmidhiy (02/133) amepokea sehemu ya mwisho kutoka kwake na Ibn Maajah kupitia kwa Qataadah. at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri.”

Bali ni Hadiyth Swahiyh. Hakika cheni ya wapokezi wake kutoka kwa Jaabir ni Swahiyh[2]. Itakuweje ikiwa itaunganishwa na Hadiyth ya Abu Qataadah? Swiddiyq Hasan Khaan katika “ar-Rawdhwat-un-Nadiyyah” (01/164) kwa Muslim ambapo akakosea katika hilo.

Ziada ni ya Ahmad katika upokezi wake.

Wanachuoni wamesema:

“Makusudio ya kuifanya vizuri sanda yake ni ule usafi wake, ukubwa wake na imsitiri. Makusudio sio kufanya israfu kwayo, ughali wake na kushindana kwayo.”

Kuhusu ile sharti iliowekwa na an-Nawawiy katika “al-Majmuu´” (05/195 na 197) kwamba iwe katika aina ya yale mavazi yake wakati wa uhai wake kwa njia ya kwamba isiwe ya fakhari zaidi wala duni kuliko ilivyokuwa ni jambo ambalo lina mtazamo kwangu mimi. Kwa sababu, pamoja na kwamba ni miongoni mwa mambo yasiyokuwa na dalili, mavazi yake wakati wa uhai wake pengine yalikuwa ni ya fakhari au ya duni, ni vipi basi sanda yake iwe katika aina hiyo?

36- Ikiwa sanda imekuwa ni dhiki juu ya hilo na isweze kuenea basi atafunikwa kichwa chake na kilichorefuka katika kiwiliwili chake. Sehemu itayobaki wazi itawekwa kitu katika yale majani ya al-Idhkhira au majani mengineyo. Kuhusiana na hilo kuna Hadiyth mbili:

Ya kwanza: Khabbaab bin al-Aratt juu ya kisa cha Musw´ab na maneno yake kuhusu ile nguo yake:

“Iwekeni katika ile sehemu kuanzia kichwa chake [Katika upokezi mwingine imekuja: “Mfunikeni kwayo kichwa chake] na wekeni juu ya miguu yake majani ya al-Idhkhira.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim. Imekwishatangulia kwa ukamilifu wake katika masuala ya 34 ukurasa wa 57.

Ya pili: Haarithah bin Mudhwarriy ameeleza:

“Niliingia kwa Khabbaab na amechomwa [katika tumbo lake] mara saba. Akasema: “Lau kama mimi sikumsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema: “Asitamani mmoja wenu mauti” basi ningeliyatamani. Hakika mimi nimejiona pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) similiki dirhamu. Hakika pambizoni mwangu mwa nyumba yangu hivi sasa kuna dirhamu elfu arubaini kisha akaleta sanda yake. Wakati alipoiona akalia na akasema: “Lakini Hamzah hakukupatikana kwake sanda isipokuwa kiguo cheupe chenye misitarisitari ambacho pindi kilipokuwa kinawekwa kichwa mwake basi miguu yake hubaki wazi na pindi kilipokuwa kinawekwa miguuni mwake basi kichwa chake hubaki wazi. Hivyo miguuni mwake kukawekwa majani ya al-Idhkhira.

Ameipokea Ahmad (06/395) kwa ukamilifu huu. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. Ameipokea vilevile at-Tirmidhiy pasi na maneno: “… kisha akaleta sanda yake… “ ambaye amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

al-Bukhaariy na Muslim na wengineo wameipokea kwa njia nyingine kuhusu kutangaza juu ya kifo cha maiti.

Vilevile Hadiyth hii ina nyingine yenye kuitolea ushahidi kutoka katika Hadiyth ya Anas. Tunaitaja –Allaah akitaka – katika masuala yanayofautia:

[1] Ni majani yanayojulikana yenye harufu nzuri.

[2] Iko na njia nyingine kutoka kwa Jaabir. Ameipokea yeye na ilioko kabla yake katika ”al-Mustadrak” (01-369). Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 76-79
  • Imechapishwa: 24/02/2020