41. Wanawafadhilisha wasomi juu ya wanazuoni

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Ni jambo lisilowezekana pia kwamba wale waliokuja nyuma wakawa ni wajuzi zaidi kuliko watanguliaji, kama wanavosema baadhi ya wapumbavu ambao hawajui hadhi ya Salaf. Bali hawana maarifa kumuhusu Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waumini vile ipasavyo na wanadai kwamba mfumo wa Salaf umesalimika zaidi, lakini hata hivyo mfumo wa waliokuja nyuma ni mjuzi na wenye hekima zaidi.

MAELEZO

Suala hili ni kuhusu tofauti ya elimu ya Salaf na elimu ya wale waliokuja nyuma. Je, Salaf walikuwa wajuzi zaidi kuliko wale waliokuja nyuma au wale waliokuja nyuma ndio wajuzi zaidi kuliko Salaf? Shaykh (Rahimahu Allaah) amelizungumzia suala hili katika fatwa hii. Miongoni mwa wengine wako waliolizungumzia ni Haafidhw Ibn Rajab katika kitabu chake ”Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf”[1]. Ni jambo muhimu sana. Kwa sababu wapo wanaodai kuwa waliokuja baadaye ni wajuzi zaidi kuliko Salaf na kwamba Salaf walikuwa ni wafanya ´ibaadah tu na wenye kuwatakia watu mema lakini hata hivyo hawakubobea na kuzama ndani elimu tofauti na walivyofanya wale waliokuja nyuma. Kwa mujibu wa watu hawa eti wale waliokuja nyuma wamezama, wakajenga dalili na wakaja na elimu ya mantiki, falsafa na mijadala – kwa hiyo wao walikuwa wajuzi zaidi kuliko Salaf katika kipengele hichi. Shaykh (Rahimahu Allaah) na wengine wanaraddi nadharia hii, kwa sababu kwanza ni upotofu, pili ni kuwatia Salaf katika upotofu na katika ujinga.

Fikira hii ipo hii leo ambapo kuna watu wanawatia wanazuoni katika ujinga na wanasema kuwa hawafahamu kitu, hawana uelewa juu ya mambo ya kisasa (فقه الواقع), kwamba hawazijua hali za watu na kuwa hawajui mambo ya kisiasa. Aidha wanadai kuwa waandishi, wasomi na wafikiriaji ndio wanaofahamu na wenye ujuzi wa mambo hayo. Wanawafadhilisha wasomi juu ya wanazuoni. Kila watu wana warithi wao.

[1]

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaaa al-Hamawiyyah, uk. 73-74
  • Imechapishwa: 06/08/2024