41. Swalah ya ijumaa haisihi isipokuwa nyuma ya imamu mwadilifu?

Swali 41: Ni ipi hukumu ya watu ambao hawaswali ijumaa kwa hoja eti haisilihi isipokuwa nyuma ya imamu mwadilifu[1]?

Jibu: Allaah (Subhaanah) amewawajibishia waislamu kutekeleza swalah ya ijumaa wakiwa ni wenyeji. Ni mamoja wakiwa katika mji mkubwa au kijiji. Wanazuoni wametofautiana katika maoni mengi kuhusu idadi ambayo ni sharti ili kuweze kusimamishwa swalah ya ijumaa. Maoni yenye nguvu ni kwamba inaswaliwa kwa idadi ya watu watatu na zaidi ya hapo kwa kutokuwepo dalili ya kushurutisha zaidi ya idadi hiyo. Wameafikiana juu ya kwamba sio sharti imamu awe mwadilifu au aliyekingwa na makosa. Bali ni lazima itekelezwe pamoja na mwema na muovu muda wa kuwa ni muislamu na uovu wake haujamtoa nje ya Uislamu.

Kwa haya inapata kufahamika kwamba kundi ambalo haliswali swalah ya ijumaa eti kwa sharti imamu awe mwadilifu au aliyekingwa na makosa wamezua ndani ya dini yale ambayo Allaah hakuyaidhinisha. Wameweka sharti ambayo haina msingi wowote katika Shari´ah takasifu.

Baadhi ya wanazuoni walikuwa wakiona kuwa swalah ya ijumaa haitekelezwi katika vijiji vidogo na kwamba inatekelezwa katika miji mikubwa inayokusanya. Lakini maoni haya ni dhaifu na hayana msingi wowote katika Shari´ah takasifu. Eti imepokelewa kutoka kwa kiongozi wa waumini ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh). Lakini hata hivyo haikusihi kutoka kwake. Swalah ya ijumaa iliswaliwa Madiynah baada ya waislamu wa mwanzo kuhamia huko na kipindi hicho ulikuwa mji mdogo. Kisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pia akaiswali wakati alipofika Madiynah na ikaendelea kuswaliwa mpaka alipofariki (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bahrayn, katika kijiji kinachoitwa ´Jawaathaa`, iliswaliwa swalah ya ijumaa zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakukataza hilo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kwa kumalizia ni kwamba ni lazima kutekeleza swalah ya ijumaa katika miji na vijiji kwa kufanyia kazi dalili za Shari´ah kutoka katika Qur-aan na Sunnah na kupata manufaa makubwa yanayopatikana kwa kuisimamisha. Miongoni mwa manufaa hayo ni kuwakusanya watu juu ya kheri, kuwawaidhi, kuwakumbusha, kuwafunza yale yenye kuwanufaisha, kujuana, kusaidiana katika wema na kumcha Allaah na mengineyo.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/342-344).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 80-81
  • Imechapishwa: 04/12/2021