41. Nguzo ya tatu ya swalah ni kusoma al-Faatihah

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema:

Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Nguzo ya tatu ni kusoma “al-Faatihah” nayo ni nguzo katika kila Rak´ah. Kama ilivyo katika Hadiyth:

“Hana swalah kwa yule asiyesoma ufunguzi wa kitabu.”

Nayo ndiyo mama wa Qur-aan.

MAELEZO

Kusoma al-Faatihah katika kila Rak´ah ya swalah ni wajibu kwa imamu, maamuma na anayeswali peke yake. Hilo ni kutokana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hana swalah yule ambaye ufunguzi wa Kitabu.”

Ameipokea al-Bukhaariy (756) na Muslim (393).

Maamuma anaisoma nyuma ya imamu wake katika swalah ya kusoma kimyakimya na ya kusoma kwa sauti ya juu. Dalili ya kuisoma nyuma ya imamu wake katika swalah za kusoma kwa sauti ya juu ni Hadiyth ya bwana mmoja miongoni mwa Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ameleeza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pengine nyinyi mnasoma nyuma ya imamu wakati imamu yuko anasoma?” Wakasema: “Ndio, tunafanya hivyo.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Basi msifanye hivyo, isipokuwa mmoja wenu asome mama wa Kitabu” au alisema “Ufunguzi wa Kitabu.”

Ameipokea Ahmad katika ”Musnad” (18070) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Kumepokelewa mfano wa hiyo kupitia kwa ´Ubaadah bin as-Swaamitw (Radhiya Allaahu ´anh). Katika cheni yake ya wapokezi yupo Muhammad bin Ishaaq, ambaye ametaja wazi kuwa amesimulia Hadiyth hiyo. Hivyo imeondoka khofu ya udanganyifu wake. Ameipokea Ahmad katika ”Musnad” (22745).

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 47-49