Tambueni kwamba Allaah amemuhalalishia mwenye kufunga kujistarehesha na mke wake katika usiku wa swawm. Allaah (Subhaanah) amesema:

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ

“Mmehalalishiwa usiku wa swawm kujamiiana na wake zenu… “[1]

Neno (الرفث) ni kinaya cha jimaa. Imesemekana vilevile ya kwamba neno (الرفث) linalojumuisha kila analolitaka mwanaume kutoka kwa mke wake. Vyovyote ilivyo, kuuhusisha ruhusa huo na usiku pekee ni dalili ya kuharamishwa kwake kwa mfungaji katika mchana wa swawm. Tayari imeelezwa yaliyowekwa kwa yule anayefanya jimaa katika mchana wa swawm wa Ramadhaan katika kafara nzito. Haya yote yanamsisitiza muislamu ajiepushe na mambo yanayomuingiza katika khatari na yanayoharibu swawm yake.

2 – Aina ya pili ya kifunguzi cha swawm ni kutoka kwa manii bila jimaa, bali kwa sababu ya kubusu, kugusana, kujichua au kwa kutazama mara kwa mara. Ikiwa mwenye kufunga atatoa manii kwa sababu ya mojawapo ya mambo haya, basi funga yake huharibika. Inamlazimu ajizuilie kula na kunywa sehemu ya mchana iliyobaki na alipe siku hiyo iliyotokea jambo hilo. Hakuna kafara juu yake, lakini inamlazimu atubie, ajutie, aombe msamaha na ajiepushe na mambo haya yanayochochea matamanio, kwa sababu yuko katika ´ibaadah kubwa sana. Ilimpasa aache matamanio yake, chakula chake na kinywaji chake kwa ajili ya Mola wake (´Azza wa Jall).

Ama aliyelala kisha akaota ndoto ya kujamiiana na akatoa manii, jambo hilo halina athari juu ya swawm yake wala hakuna kinachomlazimu, kwa kuwa limetokea bila ya kutaka kwake. Lakini inamlazimu kuoga janaba kama inavyojulikana.

[1] 02:187

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 40
  • Imechapishwa: 11/03/2026