Kuhusiana na haki za wanandoa, kuna haki kabla ya uchumba, wakati wa uchumba, wakati wa kufunga pingu za maisha na wakati kumeshahakikishwa kufunga pingu za maisha katika kipindi cha ndoa.

Moja miongoni mwa haki za ndoa kabla ya uchumba uchaguzi wa mume na mke uwe umejengwa juu ya dini, wema na tabia njema. Mwanaume apendelee kuoa mwanamke kutokana na wema wake, dini yake na tabia yake njema. Mwanamke apendelee kuolewa na mwanaume kutokana na wema wake, dini yake na tabia yake njema. Kwa sababu mambo haya ndio ufunguo wa kheri na furaha. Mwenye kukosa dini hana kheri. Hakuna kheri yoyote kwa yule asiyekuwa na dini hata kama atakuwa na mambo mengine yote yanayoleta furaha. Ndio maana Mola Wetu (Subhaanahu wa Ta´ala) Amesema:

يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ

“Allaah Atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu.”[1]

Allaah Amefanya kunyanyuliwa kwa daraja za juu zaidi ni kupitia elimu ikiwa pamoja na imani. Kheri haiwezi kupatikana isipokuwa kwa dini. Ikikosekana dini vilevile kheri hukosekana. Uzuri haunufaishi maisha ya ndoa pasina dini. Mali na nasabu havinufaishi vilevile pasina dini. Ukiongezea juu ya hilo ni lazima dini iwe imeambatana na tabia njema. Maisha ya ndoa ni njia ndefu ilio na mahitajio yake na mshikamano wa milele. Ili maisha ya ndoa yaweze kuwa na nguvu na kuendelea yanahitajia yawe yamejengwa juu ya dini na tabia njema.

[1] 58:11

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 23/03/2017