Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na kila Bid´ah ni upotevu…”

Amechukua kutoka kwenye Hadiyth:

“Tahadharini na mambo mepya, kwani hakika ya kila jambo jipya ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

Kila Bid´ah, ndogo kubwa, ni upotevu pasina shaka. Mwenye kusema kinyume na hivi basi ameenda kinyume na Hadiyth ilio wazi kabisa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa akisema hivo karibu katika kila Khutbah:

“Hakika bora ya maneno ni Maneno ya Allaah na uongofu bora ni uongofu wa Muhammad. Mambo maovu kabisa ni yale mepya. Kila jambo jipya ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

Imepokelewa na Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh). Alikuwa akisema hivo katika mnasaba wa Khutbah yake ambapo ghadhabu zinakuwa kali, sauti yake inapanda na macho na uso wake unakuwa mwekundu. Kana kwamba anatahadharisha jeshi na kusema:

“Asubuhi na jioni!”

Anakuwa hivo kutokana na khatari ya Bid´ah katika Ummah. Mwenye kusema kwamba kuna Bid´ah nzuri na Bid´ah mbaya anaenda kinyume na maneno ya yule ambaye hazungumzi kwa matamanio yake. Kuna ambao wanaigawa Bid´ah katika ya wajibu, iliyopendekezwa, yenye kuchukiza na ya haramu; katika hukumu tano. Hili ni kosa. Hukumu haiwezi kuwa isipokuwa kwa dalili. Ikiwa kuna dalili ya hilo basi haiwezi kuwa Bid´ah. Ikiwa kuna dalili ya mapendekezo yake haiwezi kuwa Bid´ah. Katika hali hiyo inakuwa Sunnah. Kitendo hicho kinakuwa Sunnah na sio Bid´ah. Mgawanyo huu ni wa kimakosa waziwazi.

[1] Muslim (867).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 367
  • Imechapishwa: 31/03/2017