174 – Abul-Hasan Ahmad bin al-Husayn bin ´Abdillaah at-Tamiymiy ametukhabarisha: Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan adh-Dhahabiy ametuzindua: Muhammad bin Haaruun al-Hadhwramiy ametuhadithia: Abu Bakr Ahmad bin Muhammad bin Anas ametuhadithia: ´Abdul-Wahhaab bin Naafiy´ ametuhadithia: al-Fadhwl bin Ibraahiym ametuhadithia, kutoka kwa Mu´aawiyah bin Qurrah, kutoka kwa Anas bin Maalik: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika mtu ambaye atakuwa na hesabu nzito siku ya Qiyaamah ni yule aliyetoshelezwa na alikuwa na wakati.”[1]

175 – Abul-Qaasim ´Abdur-Rahmaan bin ´Ubaydillaah al-Harbiy ametukhabarisha: Abu Bakr Ahmad ibn Salmaan an-Najjaad ametuhadithia: Ja´far as-Swaa-igh ametuhadithia: ´Affaan ametuhadithia: ´Awn bin Ma´mar ametuhadithia, kutoka kwa al-Jald bin Ayyuub, kutoka kwa Mu´aawiyah bin Qurrah, ambaye amesema:

”Hakika mtu ambaye atakuwa na hesabu nzito siku ya Qiyaamah ni yule aliyekuwa mzima na alikuwa na wakati.”

176 – al-Hasan bin Abiy Bakr ametukhabarisha: ´Uthmaan bin Ahmad ad-Daqqaaq ametukhabarisha: Haydhwaam bin Qutaybah al-Marwaziy ametuhadithia: Muhammad bin Kulayb ametuhadithia: Ismaa´iyl bin ´Ayyaash ametuhadithia: Mutw´im bin al-Miqdaam as-Swan´aaniy na wengine wametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin Waasiy´ al-Azdiy, aliyesema:

”Abud-Dardaa´ alimwandikia Salmaan: ”Kutoka kwa Abud-Dardaa´ kwenda kwa Salmaan. Ndugu kipenzi! Itumie vizuri afya na wakati wako kabla ya kupatwa na mtihani ambao hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kukuondoshea nao.”

177 – al-Husayn bin ´Umar bin Burhaan al-Ghazzaal ametukhabarisha: Abul-Husayn ´Abdul-Baaqiy´ bin Qaaniy´ bin Marzuuq al-Qaadhwiy alituhadithia kwa njia ya kututaka kuandika: Bishr bin Muusa ametuhadithia: ´Abdullaah bin Swaalih ametuhadithia: Yahyaa bin Humayd ametuhadithia: al-Awzaa´iy alimwandikia mmoja katika ndugu zake:

”Umezungukwa kutokea kila upande na huko unapelekwa kila siku. Kwa hiyo hakikisha unajihadhari na Allaah na kusimama mbele Yake.”

178 – Muhammad bin Ahmad bin Rizq ametukhabarisha: Ja´far bin Muhammad bin Naswr al-Khuldiy ametukhabarisha: Muhammad bin ´Abdillaah al-Hadhwramiy ametuhadithia: ´Abdullaah bin Khubayq ametuhadithia: Ishaaq bin ´Abdil-´Aziyz ametuhadithia, kutoka kwa ´Atwaa’ bin Muslim, aliyesema:

”Nilikuwa pamoja na Sufyaan ath-Thawriy kwenye msikiti Mtakatifu. Akasema: ”Ee ´Atwaa´! Sisi tumeketi ilihali mchana unafanya kazi yake.” Nikasema: ”Mimi niko katika kheri – Allaah akitaka.” Akasema: ”Ni kweli, lakini muda unaondoka. Ee ´Atwaa´! Wakati muumini katika uwanja wa Mkusanyiko atapoyaona yale ambayo Allaah amemwandalia Peponi, basi atatamani lau kama kamwe asingeliumbwa kutokana na aliyomo.”

179 – Abu ´Abdillaah al-Husayn bin al-Hasan bin Muhammad bin al-Qaasim al-Makhzuumiy ametukhabarisha: Muhammad bin ´Amr ar-Razzaaz ametukhabarisha: Hanbal bin Ishaaq, binamu yake Ahmad bin Hanbal, ametukhabarisha: Abul-Waliyd Khalaf bin al-Waliyd ametuhadithia: Mmoja katika binamu zake Abu Bakr an-Nahshaliy amenihadithia:

”Ibn-us-Sammaak alimtembelea Abu Bakr an-Nahshaliy akiwa sokoni. Alikuwa ameinamisha kichwa chake chini na akiswali kwa kuashiria. Ndipo akasema: ”Allaah ametakasika na mapungufu! Hii ndio hali?” Akasema: ”Ee Ibn-us-Sammaak! Naharakisha kabla ya kufungwa daftari langu la matendo.”

[1] Dhaifu mno kwa sababu ya ´Abdul-Wahhaab bin Naafiy´ al-´Aamiriy al-Mutwawwa´iy. ad-Daaraqutwniy: ”Ni mnyonge sana”. Vilevile sijapata wasifu wa al-Fadhwl bin Ibraahiym. Ni kweli kwamba al-Jald bin Ayyuub amemfanyia ufuatiliaji kupitia kwa Mu´aawiyah bin Qurrah, kama itakavyokuja katika Hadiyth inayofuata, lakini kwa njia ya Mu´aawiyah mwenyewe, jambo ambalo ndio karibu zaidi na usahihi. Ingawa al-Jald mwenyewe huyu ameachwa, kama alivosema ad-Daaraqutwniy.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr Ahmad bin ´Aliy al-Khatwiyb al-Baghdaadiy (afk. 463)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Iqtidhwaa’-ul-´Ilm al-´Amal, uk. 100-102
  • Imechapishwa: 26/05/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy