38. Wanafunzi wa Maswahabah waliopangusa juu ya soksi

Si jambo lililofichika kwamba ikiwa katika suala fulani hayakupatikana masimulizi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka kwa Maswahabah na ikapatikana maoni au fatwa ya mwanafunzi wa Maswahabah katika jambo hilo, basi hilo huzingatiwa au huathiri, khaswa katika mlango wa kumfuata aliye na elimu zaidi na ubora zaidi kwa wale wanaofuata kibubusa. Muhammad bin Sa´d[1]  amepokea kwamba Abu Salamah bin ´Abdir-Rahmaan alimwambia al-Hasan:

”Je, yale unayowatolea watu fatwa ni jambo ulilolisikia au ni maoni yako mwenyewe?” al-Hasan akasema: ”Hapana, naapa kwa Allaah, kwamba si kila tunalolitolea fatwa tumelisikia. Bali maoni yetu kwao ni bora kuliko maoni yao wenyewe.”[2]

Imepokelewa masimulizi kadhaa kutoka kwa wanafunzi wa Maswahabah kuhusu kupaka juu soksi. Imaam Ibn Hazm amesimulia ”al-Muhallaa”, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa Sa´iyd ibn al-Musayyib, ambaye amesema:

”Sokzi za kawaida ni sawa na soksi za ngozi katika kupaka juu yake.”

Ibn Jurayj amesema:

”Nilimwambia ´Atwaa: ”Je, kunapakwa juu ya soksi za  kawaida?” Akasema: ”Ndiyo. Zipakeni kama soksi za ngozi.”

Ibraahiym an-Nakha´iy alikuwa haoni ubaya wowote wa kupangusa juu ya soksi za kawaida.

al-Fadhwl bin Dukayn amesema:

”Nilimsikia al-A´mash akiulizwa kama inaruhusiwa kwa aliyelala kupangusa juu ya soksi. Akijibu: ”Ndiyo.”

Qataadah amesimulia kutoka kwa al-Hasan na Khilaas bin ´Amr kwamba walikuwa wakiziona soksi za kawaida katika kupaka juu yake kuwa ni sawa na soksi za ngozi. Kisha akawataja miongoni mwa wanafunzi wa Maswahabah Sa´iyd bin Jubayr na Naafiy´[3]. Kisha Ibn Hazm akasema:

”Na hayo ndio maoni ya Sufyaan ath-Thawriy, al-Hasan bin Hayy, Abu Yuusuf, Muhammad bin al-Hasan, Abu Thawr, Ahmad bin Hanbal, Ishaaq bin Raahawayh, Daawuud bin ´Aliy (adh-Dhwaahiriy) na wengineo.”

[1] Mtunzi wa kitabu “at-Twabaqaat al-Kubraa”.

[2] I´laam-ul-Muwaqqi´iyn (1/75).

[3]  Ameipokea bn Abiy Shaybah (1/189) kutoka kwa Sa´iyd bin al-Musayyab, Sa´iyd bin Jubayr, Naafiy´ na Ibraahiym kwa matamshi yanayofanana na hayo ambayo yameshatangulia. ´Atwaa´ amesema:

”Kupangusa juu ya soksi za kawaida ni kama kupangusa juu ya soksi za ngozi.”

Cheni yake ya wapokezi ni Swahiyh.

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 62-63
  • Imechapishwa: 15/04/2026