Miongoni mwa yanayothibitisha tuliyotanguliza kuhusu nadharia ya kupata ni yale as-Suyuutwiy mwishoni mwa utafiti wake kuhusu Hadiyth Swahiyh:

”Kwa mujibu wa Imaam Ibn Burhaan katika ”al-Awsatw” ni kwamba wanazuoni wote wa Fiqh wameona kuwa kufanyia kazi Hadiyth hakutegemei kule kusikia pekee; bali ikiwa nakala imethibiti kwake, basi inajuzu kwake kuitendea kazi hata kama hakuisikia.”[1]

Abu Ishaaq al-Isfaraayiyniy amenukuu maafikiano juu ya kujuzu kunukuu kutoka katika vitabu vinavyotegemewa na kwamba haishurutishwi kuungana kwa cheni ya wapokezi hadi kwa watunzi wake. Ilkiyaa at-Twabariy amesema wakati alipokuwa analitolea hilo maelezo:

”Mwenye kukuta Hadiyth katika kitabu sahihi inajuzu kwake kuisimulia na kuitolea hoja.”

Shaykh ´Izz-ud-Diyn bin ´Abdis-Salaam amesema wakati alipokuwa anajibu swali:

”Ama kutegemea vitabu sahihi vya Fiqh vinavyoaminika, wanazuoni katika zama hizi wameafikiana juu ya kujuzu kuvitegemea na kurejea kwavyo, kwa kuwa uaminifu umepatikana kwa hivyo kama unavyopatikana kwa riwaya. Kwa sababu hiyo watu wametegemea vitabu mashuhuri katika sarufi, lugha, tiba na elimu nyingine kwa kupatikana uaminifu kwake na kuwa mbali na udanganyifu.”

Basi zingatia kuafikiana kwa maneno ya maimamu juu ya kutegemea yaliyomo ndani ya vitabu vya Fiqh na vinginevyo, basi utajua kwamba ikiwa ndani yake kunapatikana kunukuu kutoka kwa Swahabah au kusimuliwa madhehebu yake, basi huaminika na hufanyiwa kazi bila shaka. Maoni kama hayo yanakuwa ni bora zaidi kuliko vinginevyo katika mlango wa kufuata kibubusa kwa mwenye kutaka hivyo. Basi elewa wala usiwe mfungwa wa kufuata kichwa mchunga.

[1] Tadriyb-ur-Raawiy, uk. 49.

  • Muhusika: ´Allaamah Muhammad Jamaal-ud-Diyn bin Muhammad al-Qaasimiy (afk. 1332)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mash ´alaal-Jawrabayn, uk. 61-62
  • Imechapishwa: 15/04/2026