38. Swalah ya ijumaa nyuma ya watawala

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Swalah ya ijumaa nyuma yao na nyuma ya magavana wao inafaa na ni timilifu na ni Rak´ah mbili. Yule mwenye kuirudi ni mtu wa Bid´ah mwenye kuyaacha mapokezi na anaenda kinyume na Sunnah. Hapati chochote katika fadhila za ijumaa midhali haonelei kuwa ni sahihi kuswali swalah ya ijumaa nyuma ya viongozi sawa wawe wema au waovu. Sunnah ni kuswali Rak´ah mbili pamoja nao na kuonelea kuwa ni timilifu. Usiwe na shaka kwenye kifua chako juu ya hilo.”

MAELEZO

 Swalah ya ijumaa, swalah za mkusanyiko na swalah za ´iyd mbili ni lazima kuziswali nyuma ya watawala. Yule mwenye kuonelea kwamba kuswali swalah ya ijumaa nyuma ya kiongozi aliyepo si sahihi na kwamba inasihi tu kuswali nyuma ya ambaye amekingwa na makosa kutoka katika familia ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama ilivyo kwa Shiy´ah na wale wafuasi wao, ni mpotevu. Haifai kuiga fikira hii. Haifai kutilia shaka kwamba swalah ya ijumaa nyuma ya mtawala Rak´ah mbili ni sahihi, ni mamoja mtawala huyo ni mwema au mwovu. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 141-142
  • Imechapishwa: 30/04/2019