Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Baada ya watu wa mashauriano wanakuja Muhaajiruun walioshiriki katika vita vya Badr, kisha Answaar walioshiriki katika vita vya Badr; kila mmoja kwa mujibu wa kuhajiri na kutangulia kwake katika Uislamu.

MAELEZO

Hapana shaka yoyote kwamba Maswahabah bora ni wale makhaliyfah waongofu Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum). Makhaliyfah waongofu ni Abu Bakr, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan na kisha ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhum). Kuna maafikiano juu ya mpangilio huu.

Watu wa mashauriano ni wale watu sita ambao waliteuliwa kumchagua khaliyfah baada ya ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhum).

Kisha wanafuata wale waliopambana vita vya Badr. Halafu wanafuata wale waliokula kiapo chini ya mti. Kisha Maswahabah waliohajiri, wakajitolea mali zao na wakapambana kabla ya kuhajiri na hatimaye wale waliohajiri, wakajitolea mali zao na wakapambana baada ya kuhajiri. Kwa maana nyingine ni wenye kutofautiana katika ubora, kama ilivyothibiti ndani ya Qur-aan na Sunnah.

Wanaposema wanazuoni yale yanayofahamishwa na Maandiko juu ya kutofautiana kiubora haina maana kuwa wanatiwa mapungufu Maswahabah wengine. Kila mmoja mmoja ana ujira wake. Kila mmoja ana sifa zake za kipekee, wote ni Maswahabah. Wote wana ubora wa kuwa Maswahabah. Ambaye alimuona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kumuamini, ijapo ni kwa muda wa kupepesa macho, ni katika Maswahabah. Haijalishi kitu yale matendo mema yatayofanywa na wale waliokuja baada yao hawana daraja ya ubora sawa na Maswahabah. Kwa sababu hakuna ubora wowote unaolingana na ubora wa uswahaba.

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 109