Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Mbora wa Ummah huu baada ya Mtume wake ni Abu Bakr as-Swiddiyq, kisha ´Umar bin al-Khattwaab halafu ´Uthmaan bin ´Affaan. Tunawatanguliza hawa watatu kama walivyotangulizwa na Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hawakutofautiana juu ya hilo.

Baada ya hawa watatu ni wale wa mashauriano watano: ´Aliy bin Abiy Twaalib, az-Zubayr, ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Sa´d na Twalhah. Wote walikuwa wanastahiki ukhaliyfah na wote walikuwa viongozi. Dalili yetu juu ya hilo ni maneno ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Tulikuwa, ilihali Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado yuhai,  tukizingatia ya kwamba Abu Bakr ndiye bora na halafu ´Umar, kisha ´Uthmaan. Kisha tunanyamaza.”

MAELEZO

Hawa ndio makhaliyfah watatu wema, wachaji na wabora. Wako katika mpangilio huu wa ukhaliyfah na ubora. Abu Bakr ndiye khaliyfah wa kwanza mbora na mwongofu, kisha anafuata ´Umar katika ubora na ukhaliyfah, kisha ´Umar ndiye anayefuata katika ubora na ukhaliyfah, halafu ´Aliy  bin Abiy Twaalib ndiye anayefuata katika ubora na ukhaliyfah, baada ya kuapishwa kama khaliyfah.

Wanazuoni wanaozingatiwa wameafikiana kwamba mpangilio wao katika ukhaliyfah ndio mpangilio wao katika ubora. Wanatofautinaa na Raafidhwah ambao wanaochupa mipaka juu ya ´Aliy bin Abiy Twaalib na watu wa nyumbani kwake. Raafidhwah ni waongo na mazanadiki. Wanahukumu kwa matamanio yao na wana I´tiqaad za khatari zinazotilia nguvu ukafiri wao mbaya. Yule anayetaka kujua zaidi arejee vitabu vinavyozungumzia dini na mapote.

Wanatofautiana pia na Khawaarij wakosefu wa adabu wanaomkufurisha ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na wale waliosimama pamoja naye. Khawaarij ni watu wenye uadui na waasi ambao wanawakufurisha watu kwa dhuluma na uadui.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni watu wa kati na kati, baina ya Raafidhwah na Khawaarij, na wanatambua ukhaliyfah wa wale makhaliyfah wanne kwa mpangilio unaotambulika. Wakati ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alipoaga dunia watu wa mashariano wakamchagu ´Uthmaan ndiye ambaye atachukua nafasi yake. Hakuna yeyote ambaye aliona kinyume. Baada ya hapo kukatokea fitina na maoni ya Ahl-us-Sunnah juu ya jambo hilo yanatambulika; aliyepatia ana ujira mara mbili na aliyekosea ana ujira mara moja na kosa lake ni lenye kusamehewa. Kwa hiyo haifai kwa yeyote kumtukana Mu´aawiyah, Twalhah, az-Zubayr, ´Aliy bin Abiy Twaalib na wale waliokuwa pamoja nao. Haijuzu kwa yeyote kutoa maoni yake juu ya magomvi yaliyotokea baina yao. Hivo ndivo ilivyo ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Wanawaheshimu wabwana wakubwa hao na wanajaribu kufasiri kuteleza kwao kwa njia bora kabisa iwezekanayo. Wanasema juu yao yale yaliyosemwa na Salaf wa mwanzo: aliyepatia ana ujira mara mbili na aliyekosea ana ujira mara moja na kosa lake ni lenye kusamehewa. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wote imethibiti juu ya msingi huu.

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 103-105at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah
  • Imechapishwa: 12/05/2026