Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya utegemeaji ni maneno Yake (Ta´ala):

وَعَلَى اللَّـهِ فَتَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Na kwa Allaah pekee tegemeeni ikiwa nyinyi ni waumini.” (al-Maaidah 05 : 23)

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Na yeyote yule atakayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.” (at-Twalaaq 65 : 03)

MAELEZO

Kutegemea kitu ni kule kukiamini na kukiegemea. Kumtegemea Allaah (Ta´ala) ina maana ya kumtegemea Allaah (Ta´ala) pekee ili kuleta manufaa na kuzuia madhara. Kitendo hichi ni katika kukamilika na alama ya imani. Amesema (Ta´ala):

وَعَلَى اللَّـهِ فَتَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Na kwa Allaah pekee tegemeeni ikiwa nyinyi ni waumini.”

Mja akiwa mkweli katika kumtegemea Kwake Allaah (Ta´ala), basi humtosheleza kwa kile anachohitajia. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Na yeyote yule atakayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.”

bi maana atamtosheleza yeye. Kisha Akamtuliza yule mtegemeaji na kusema:

إِنَّ اللَّـهَ بَالِغُ أَمْرِهِ

“Hakika Allaah anatimiza amri Yake.” (at-Twalaaq 65 : 03)

bi maana hashindwi na kitu chochote anachokitaka.

Tambua kwamba kutegemea kumegawanyika sampuli mbalimbali:

1- Kumtegemea Allaah (Ta´ala) ambako ni katika ukamilifu wa imani na alama ya ukweli wake. Hii ni wajibu na imani haitimii isipokuwa kwayo. Kumeshatangulia dalili yake.

2- Kutegemea kwa siri ambako kunamfanya mtu akamtegemea mfu ili kuleta manufaa au kuzuia madhara. Hii ni shirki kubwa, kwa sababu haitokei isipokuwa kwa yule mwenye kuitakidi kwamba mfu huyu ana uendeshaji wa siri katika ulimwengu. Jengine ni kwamba hakuna tofauti ikiwa mfu huyo atakuwa ni Mtume, walii au shaytwaan ambaye ni adui wa Allaah (Ta´ala).

3- Kumtegemea mwengine kwa kitu anachokiweza, pamoja na kuonelea kuwa na hadhi ya juu licha ya kuwa yeye mwenyewe hadhi yake ni ya chini. Mfano wa hilo akawa anamtegemea katika kupata riziki na mfano wa hayo. Hii ni aina ya shirki ndogo kutokana na nguvu ya moyo ulivyofungamana naye na kumtegemea.

Ama ikiwa utegemeaji wake kwake hauvuki zaidi ya kuonelea kuwa yeye ni sababu tu na Allaah (Ta´ala) ndiye amempa uwezo wa kawaida au hadhi hiyo, basi itakuwa sio shirki ikiwa mtegemewaji huyo anaweza kufanya hivo kwa njia sahihi.

4- Kumtegemea mwengine kwa kitu anachokiendesha yeye, kwa njia ya kwamba anamuwakilisha mtu mwengine afanye kitu katika nafasi yake midhali kitendo hicho kinajuzu. Hili halina neno kutokana na dalili ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Ya´quub alisema kuwaambia wanawe:

يَا بَنِيَّ اذْهَبُوا فَتَحَسَّسُوا مِن يُوسُفَ وَأَخِيهِ

“Ee wanangu! Nendeni mkamtafute Yuusuf na ndugu yake.” (Yuusuf 12 : 87)

Vilevile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwawakilisha watu kukusanya na kuihifadhi Zakaah. Vivyo hivyo aliwawakilisha watu katika kusimamisha adhabu za kidini. Alimuwakilisha ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) katika hija ya kuaga kuchinja nafasi yake na akamwambia atoe swadaqah ngozi na blanketi ya ngamia. Akamwamrisha pia kuchinja ngamia mia waliobakia baada ya yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuchinja ngamia sitini na tatu kwa mkono wake.

Ama kuhusu maafikiano kujuzisha jambo hilo, ni jambo linalotambulika kwa njia ya jumla.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 58-59
  • Imechapishwa: 22/05/2020