37. Allaah ni mkubwa kuliko kila kitu

Miongoni mwa mambo yanayomsaidia muislamu kupoteza matumaini kutaka kujaribu kuelewa namna ya sifa za Muumba (Subhaanah) ni kwamba aamini kuwa Allaah ni mkuu kuliko vingine vyote. Muislamu akiitakidi kuwa Allaah ni mkubwa kuliko kila kitu na kwamba kila kikubwa ni kidogo mbele ya ukuu na utukufu wa Allaah, basi atajua ujuzi wenye yakini ya kwamba ukuu wa Mola, utukufu, uzuri, sifa Zake ni jambo lisiloweza kufahamika kwa akili, kufikirika kwa akili au kutambuliwa kwa kuona na kwa mawazo. Allaah ni mkubwa zaidi na zaidi kuliko hivo. Bali akili na ufahamu hushindwa kuelewa viumbe vingi vya Allaah, kusemwe nini juu ya Mola (Subhaanah). Imethibiti kwamba Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Umbali kati ya mbingu ya chini kabisa na mbingu inayofuata ni miaka mia tano. Umbali kati ya kila mbingu ni miaka mia tano. Umbali kati ya mbingu ya saba na Kursiy ni miaka mia tano. Umbali kati ya Kursiy na Maji ni miaka mia tano. ´Arshi iko juu ya Maji, Allaah Yuko juu ya ´Arshi na hakuna chochote katika matendo yenu kinachojificha Kwake.”[1]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hazikuwa mbingu saba ukilinganisha na ´Arshi isipokuwa ni kama sarafu saba za fedha kwenye ngao. Kursiy ukilinganisha na ´Arshi ni kama pete ya chuma iliyotupwa kwenye jangwa.”[2]

Hebu muislamu azingatie ukubwa wa mbingu saba ukilinganisha na ardhi, ukubwa wa Kursiy ukilinganisha na ukubwa wa mbingu na ukubwa wa ´Arshi ukilinganisha na Kursiy. Sababu akili haiwezi kufahamu ukamilifu wa vitu hivi au uhalisia wake au namna yake. Itawezaje basi inapokuja kwa Muumba (Subhaanah)? Yeye ni mkubwa na ni mtukufu zaidi kusema kwamba akili iweze kutambua namna ya sifa Zake au ukubwa na utukufu Wake. Kwa ajli hiyo Sunnah ikaja kukataza kufikiria ukubwa wa Allaah, kwa sababu haviwezi kuelewa namna ya sifa Zake. Allaah ni mkubwa zaidi kuliko hivo. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Zifikirieni neema za Allaah wala msimfikirie Allaah.”[3]

[1] ad-Daarimiy katika “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah”, uk. 26-27, at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr” (9/228), Abush-Shaykh katika “al-´Adhwamah” (2/689), al-Bayhaqiy katika “al-Asmaa’ was-Swifaat” (2/290) na wengineo. al-Haythamiy amesema:

”Wasimulizi wake ni wasimulizi wa Swahiyh.” (Majma’-uz-Zawaa-id (1/86))

Swahiyh kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika “Mukhtaswar-ul-´Uluww”, uk. 100.

[2] Ibn Abiy Shaybah katika ”Kitaab-ul-´Arsh” (58), Ibn Hibbaan (361), Abush-Shaykh (259) na wengineo. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (109).

[3] al-Laalakaa’iy (3/525) na Abush-Shaykh (2/210) kupitia kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh). Cheni yake ya wapokezi ni dhaifu sana. Hata hivyo inatiwa nguvu na zingine kupitia kwa Abu Hurayrah, ´Abdullaah bin Salaam, Abu Dharr na Ibn ´Abbaas. Nzuri kupitia zingine kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (1788).

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 58-60
  • Imechapishwa: 03/12/2025

Turn on/off menu