36. Radd juu ya hoja tata za wanaokanusha Allaah kushuka katika mbingu ya chini

Kwa vile Hadiyth hii imepokelewa kwa mapokezi mengi (متواتر) na wakaona hawana namna ya kuikwepa, sasa wakataka kujibebetua ili wajikwamue nayo. Wakasema:

“Hushuka”

maana yake ni amri Yake ndio hushuka. Tunawaraddi kwa kuwaambia: katika Hadiyth imekuja ya kwamba Husema: “Ni nani anayeniomba msamaha Nimsamehe? Ni nani anayeniomba Nimpe? Kuna mwenye kutubia Nimkubalie tawbah Yake? Kuna mwenye kuniomba msamaha Nimghufurie? Kuna kwenye kuniomba Nimpe?”[1]

Je, amri inaweza kusema:

“Ni nani anayeniomba Nimpe? Ni nani anayeniomba msamaha Nimsamehe?”

Hili ni batili. Mwenye kusema haya ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Wakasema:

“Hushuka Mola wetu.”

maana yake ni Malaika miongoni mwa Malaika ndiye mwenye kushuka. Tunawaraddi kwa kuwaambia: Je, Malaika ndiye mwenye kusema:

“Ni nani mwenye kuniomba msamaha? Ni nani mwenye kuniomba? Ni nani mwenye kutubia Nimkubalie tawbah yake?”

Hivi kweli Malaika anaweza kusema haya au yanasemwa na Mola (Subhaanahu wa Ta´ala)? Bila shaka ni Mola (Jalla wa ´Alaa).

Kwa hivyo makusudio sio kwamba amri wala Malaika ndiye mwenye kushuka. Kwa kuwa si amri wala Malaika vyote viwili hakuna mwenye kuweza kutamka maneno haya yaliyotajwa katika Hadiyth.

[1] al-Bukhaariy (1145) na Muslim (168) na (758)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 97-98
  • Imechapishwa: 09/01/2024